MAGOLI 18 LIGI KUU YASHINDWA KUVUNJA REKODI

Magoli 18 yamefungwa kwenye mechi saba za ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoanza Jumamosi iliyopita, lakini yameshindwa kuvunja rekodi ya magoli ya msimu uliopita.

Kwenye mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu msimu uliopita jumla ya magoli 19 yalipatikana.

Ligi ya msimu huu imeanza kwa Azam FC kuitandika Polisi ya Morogoro mabao 3-1, Mtibwa Sugar kuichapa Yanga mabao 2-0, Stand United ya kutandikwa nyumbani mabao 4-1 dhidi ya Ndanda FC kutoka Mtwara, wakati Mgambo JKT ya Tanga iliifunga Kagera Sugar bao 1-0.

Mechi nyingine ilikuwa ni Ruvu Shooting kupata kipigo nyumbani cha mabao 2-0 kutoka kwa Prisons ya Mbeya, Mbeya City kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya JKT Ruvu, huku Simba ikibanwa mbavu katika sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union, hivyo kuzaa mabao 18.

Magoli 19 ya mechi ya ufunguzi msimu uliopita kwa mujibu wa kumbukumbu zetu yalipatikana kwa Yanga kuinyuka Ashanti mabao 5-1, Mtibwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam, JKT Oljoro ikainyuka Coastal Union mabao 2-0, Mgambo ikachapwa 2-0 dhidi ya JKT Ruvu, Simba ikatoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino ya Tabora, Mbeya City ikatoka sare ya bila kufungana dhidi ya Kagera Sugar na Ruvu Shooting ikaitandaika Prisons mabao 3-0.

Katika hatua nyingine, mchezaji wa Mgambo Shooting Ramadhani Pera ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye Ligi kuu alipofunga bao pekee dhidi ya Kagera Sugar katika dakika ya 12 kwenye raundi ya kwanza ya ligi hiyo Jumamosi.

Mabao yote yaliyopatikana kwenye mechi nyingine yalifungwa baada ya dakika hizo.

Shaaban Kisiga wa Simba anashikilia rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi katika dakika ya saba dhidi ya Coastal katika mechi ya kufunga raundi ya kwanza Jumapili.

0 comments: