Thursday, October 2, 2014

Thursday, October 02, 2014


Katuni

Watanzania waliungana na watu wengine duniani kote kuadhimisha 'Siku ya Wazee Duniani' ambayo huadhimishwa Oktoba Mosi ya kila mwaka. Katika siku hiyo, matamko mbalimbali hutolewa kwa nia ya kuikumbushia jamii juu ya wajibu wao katika kuhakikisha kwamba wazee wanapata haki zao.

Sisi tunawapongeza wazee kwa kuadhimisha siku hii. Hata hivyo, tunadhani kwamba jambo muhimu zaidi ambalo jamii inapaswa kukumbuka katika kuadhimisha siku hii ni kuhakikisha kwamba sasa kunakuwa na vitendo zaidi katika kushughulikia kero za wazee na siyo kuishia kutoa matamko na ahadi zisizokuwa na chembe ya utekelezaji.

NIPASHE tunatambua kuwa hadi sasa, masuala mengi mazuri kuhusiana na wazee yamebaki kuwa midomoni mwa jamii au kwenye nyaraka mbalimbali za serikali. Utekelezaji kuhusiana na namna ya kumaliza kero za wazee umeendelea kuwa wa chini sana na matokeo yake, wazee wetu wameendelea kukabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha.

Kwa ufupi, ni sahihi kwa wengi wao kuendelea kulalamika kuwa wametelekezwa. Jamii haiwajali kwa lishe nzuri, makazi bora, matibabu ya uhakika na ulinzi madhubuti kwa ajili ya kuwa na uhakika wa kupata haki yao ya msingi ya kuishi kama ilivyo kwa Watanzania wengine.

Kwa mujibu wa Sera ya Wazee Tanzania, mzee ni mtu mwenye umri wa miaka 60 au zaidi. Na ripoti ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa kundi hili linahusisha asilimia 5.6 ya watu Watanzania wote takriban milioni 45 waliopo nchini.

Hata hivyo, cha kusikitisha ni kwamba licha ya idadi ya wazee kuwa ndogo kulinganisha na marika mengine kama vijana, bado wazee wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi zinazotishia ustawi wa maisha yao. Yote hayo yanatokea huku taifa likiwa na rundo la nyaraka zinazozungumzia ustawi wa wazee na namna ya kushughulikia kero zao.

NIPASHE tunatambua vilevile kuwa yapo mambo kadhaa mazuri kuhusiana na wazee lakini yanakosa utekelezaji makini. Kwa mfano, kutambua changamoto zinazowakabili wazee, serikali iliandaa Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003, ambayo inajaribu kutoa majawabu kadhaa kuhusiana na kero za wazee.

Sera hii inaeleza kuwa serikali inatambua kwamba wazee ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa na inasisitiza umuhimu wa kutengwa kwa rasilimali za kutosha kwa lengo la kuboresha huduma kwa wazee; kuwashirikisha wazee katika maamuzi muhimu yanayowahusu wao na taifa kwa ujumla na kutoa ulinzi wa kisheria kwa wazee kama kundi maalum. Haya yote yanaelezwa kwenye aya ya 1.3 ya sera hiyo.

Kama hiyo haitoshi, maslahi ya wazee yamezungumziwa pia katika nyaraka nyingine nyingi kama Sera ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2003 na Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii.

Mathalan, katika Sheria Na. 1 ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2001, ibara ya 10 (1) inaruhusu Kamati ya Afya ya Kata kuidhinisha wazee kusamehewa uchangiaji kwenye mfuko huu na kupewa kadi ya utambulisho wa matibabu bora bila malipo.

Hata katika katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,  pamoja na marekebisho yake,   ibara ya 12 (2) na ibara ya 14, zinazungumzia wazee kupewa hashima na kupata hifadhi kutoka serikalini na kutoka kwa jamii.

Pamoja na wingi wa nyaraka zinazozungumzia wazee, viongozi mbalimbali pia wamekuwa hodari katika kuelezea umuhimu wa ustawi wa wazee kwa taifa. Yanatolewa matamko mengi ya kutia moyo. Hata mchakato wa katiba mpya umekuwa ukigusia umuhimu wa wazee kwani ni jambo zuri na lenye maslahi mapana ya umma. Hata hivyo, utekelezaji ni tatizo.

Kwa sababu hiyo, NIPASHE tunadhani kwamba ni vyema jamii ikakumbuka maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya wazee kwa kujielekeza zaidi katika vitendo kushughulikia kero za wazee na siyo maneno tupu. Ikumbukwe, vijana wa leo ndiyo wazee wa kesho.

CHANZO: NIPASHE     

0 comments: