Wednesday, September 30, 2015

Wednesday, September 30, 2015
Rais wa Urusi Vladimir Putin (kushoto) akisalimiana na Rais wa Marekani, Barack Obama (kulia)
Rais wa Marekani, Barack Obama amekutana na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuujadili mzozo wa Syria.

Katika hotuba zao tofauti katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo jana, Rais Obama amemtaja Rais wa Syria Bashar al Assad kama kiongozi wa kiimla anayewaua watoto huku Putin akisema ulimwengu unapaswa kumuunga mkono Assad katika kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali wa dola la kiislamu (IS) na kuonya ana mipango ya kuimarisha misaada ya kijeshi kwa utawala wa Assad.

Baada ya hotuba zao katika mkutano huo mkuu wa Umoja wa Mataifa, Obama na Putin walikutana kwa mkutano wa ana kwa ana uliodumu kwa dakika tisini, ambapo pia walikubaliana kuwa majeshi yao yanapaswa kufanya mazungumzo ili kuzuia mkwaruzano kati yao kwani majeshi yote yanafanya kampeni za kijeshi nchini Syria.

Marekani, Ufaransa na nchi washirika zinafanya mashambulizi ya angani dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS ambao wamechukua fursa ya kuwepo msukosuko nchini humo na kuyadhibiti maeneo makubwa Syria na Iraq.

Baada ya mkutano huo, Rais Putin amewaambia wanahabari kuwa nchi yake inafikiria ni njia zipi zaidi zinaweza kuisadia serikali ya Syria na wapiganaji wa Kikurdi kupambana dhidi ya IS na kuongeza kuna fursa ya kufanya kazi kwa pamoja na Marekani kushughulikia tatizo la IS.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Urusi amesema siyo wajibu wa Marekani au Ufaransa kuamua ni nani anastahili kuwa kiongozi wa Syria kwani hilo linaweza tu kuamuliwa na Wasyria wenyewe.

Rais Obama kwa upande wake amesema yuko tayari kushirikiana na Urusi na hata Iran kuvimaliza vita vya Syria, ambavyo vimedumu zaidi ya miaka minne ambapo zaidi ya watu laki mbili wameuawa na mamilioni ya wengine wameachwa bila ya makazi, lakini hakubaliani na pendekezo la kusalia madarakani kwa Rais Assad kwa madai kuwa yeye ndiye mhalifu mkubwa zaidi wa mzozo wa Syria.

Obama hakutaja moja kwa moja kuondolewa madarakani Assad na badala yake amedokeza kuwa kunaweza kuwa na kile alichokitaja kipindi cha mpito hiyo ikiwa dalili ya hivi karibuni kuwa Marekani inazingatia kumuacha Assad kubaki madarakani kwa muda, mtizamo ambao unazingatiwa na nchi za Umoja wa Ulaya.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu wamepinga uwezekano wa Assad kuruhusiwa kusalia madarakani.

0 comments: