Licha ya upinzani kutoka makundi
kadhaa ya wananchi, Bunge la Katiba jana lilihitimisha kazi yake kwa
kupitisha Katiba inayopendekezwa baada ya kupata theluthi mbili za
wajumbe wa kila upande wa Muungano.
Matokeo hayo yaliyohitimisha mchakato huo,
yalifanikishwa kwa tofauti ya kura mbili za wajumbe katika baadhi ya
ibara na nyingine kwa kura moja tu, ikimaanisha kuwa iwapo kura hizo
mbili zingekosekana hadithi ingekuwa tofauti.
Kutangazwa kwa matokeo hayo kuliwafanya wajumbe
walioshiriki mchakato hadi hatua ya mwisho baada ya wenzao wa kundi la
Ukawa kususia, kulipuka kwa furaha, nyimbo, tambo, vijembe na vigelegele
huku wakijimwaga ukumbini kusakata dansi.
Akitangaza matokeo hayo, Naibu Katibu wa Bunge
hilo, Dk Thomas Kashililah alisema hali ya upigaji kura ilikuwa ni nzuri
na kila kura za kila upande zilitosheleza na kutoa uhalali wa Katiba
inayopendekezwa kupelekwa kwa wananchi.
Katibu huyo alianza kutoa matokeo ya upande wa
Zanzibar ambako wajumbe wengi walikuwa na wasiwasi kuwa huenda usipate
akidi ya kura 146 iliyotakiwa.
Kwa jumla, kura za ‘ndiyo’ za Zanzibar zilikuwa
ama 147 au 148 na ‘hapana’ ama saba au nane; wakati kwa matokeo ya
Tanzania, wajumbe waliopiga kura walikuwa 335 na kura moja tu ndiyo
ilikataa ibara zote na kura mbili zilichomoza kukataa baadhi ya ibara.
Matokeo hayo yalithibitishwa na mawakala Amina
Makilagi na Waziri Rajabu Salum ambao walisimama na kueleza namna
ambavyo kura hizo zilihesabiwa kwa uhuru mpana.
Kuserebuka bungeni
Baada ya matokeo hayo, Ukumbi wa Bunge
ulihanikizwa kwa nyimbo za mipasho na mafumbo zikiambatana na kuwashwa
vipaza sauti bila ya utaratibu na wajumbe kurukaruka na kukumbatiana kwa
furaha.
Hali hiyo, iliwalazimu walinzi wa viongozi kuingia
ndani ya ukumbi kwa kuweka hali ya amani kwani wajumbe walianza kuvamia
viti vyao kwa nia ya kuwapongeza.
Hali ilipozidi, walinzi wa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda walimwondoa haraka na kumweka katika chumba maalumu hadi hali
ilipotulia huku idadi kubwa ya walinzi ikisogea kwa Mwenyekiti wa Bunge,
Samuel Sitta.
0 comments:
Post a Comment