Tuesday, August 25, 2015

Tuesday, August 25, 2015


Mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya (pichani kulia) amesema kuwa kwake ni fedheha kubwa kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani itakuwa sawa na kulamba matapishi yake mwenyewe.
Mkongwe huyo alitoa kauli hiyo mjini Sumbawanga, akisisitiza kuwa ni vibaya kwa mtu mzima kulamba matapishi yake mwenyewe.
“Mie kamwe siwezi kuhama CCM kwangu ni fedheha kubwa, haiwezekani maana mtu kulamba matapishi yake…wanaohama wamesahau waliyokuwa wakisema majukwaani kabla hawajawa na watu wanajua”, alisisitiza.
Alisema hakuna mtu yeyote mwenye ubavu wa kuinyoshea kidole Serikali ya awamu ya nne, kwani imefanya kazi kubwa sana labda mtu kwa hasira zake aseme vinginevyo.
Kwa makada wa CCM waliohama, aliwakumbusha kuwa walitembea nchi nzima kabla hawajajiuzulu na kumsifu Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake.
“Wanaotoka CCM na kuhamia upinzani, lazima wakumbuke kuwa walitembea nchi kabla hawajahama wakimsifu Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake majukwaani lakini ni hao hao walipoamka asubuhi wamegeuka … tena wanachosema kuwa Serikali ya Awamu ya Nne hajafanya lolote vigezo vyake ni bei ya sukari na nyama basi hakuna kingine,” alisisitiza.
Dk Mzindakaya alisema ana uhakika kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli atashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Oktoba 25.
Alitaja vigezo vitano ambavyo vitasababisha Dk Magufuli, kuibuka mshindi kwa kuwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kuongoza nchi.
“Dk Magufuli ni msafi, ni mtu mwenye uwezo wa uhakika wa kusimamia,” alisisitiza .
Alisisitiza kuwa CCM ndio chama pekee, kinachoweza kusaidia maendeleo ya nchi hii, akiwabeza wapinzani kuwa wao watabaki kutembea nchi nzima wakitukana kwani hawana jipya .
Dk Mzindakaya alisisitiza kuwa kwa hesabu zake alizopiga, CCM itashinda ubunge katika majimbo yote matano katika uchaguzi huu mkuu katika mkoa wa Rukwa ya Nkasi Kaskazini, Nkasi Kusini, Kalambo, Sumbawanga Mjini na Kwela.

0 comments: