Tuesday, August 25, 2015

Tuesday, August 25, 2015
Hali bado sio shwari katika jiji la Dar es Salaam kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa wapya 31 wa ugonjwa wa kipindupindu katika Wilaya ya Kinondoni ambapo idadi imefikia watu 47 ambao wanapatiwa matibabu katika kambi ya kipindupindu iliyopo Mburahati jijini Dar.



Mganga Mkuu wa manispaa ya Kinondoni Dk.Aziz Msuya amesema kumekuwapo na ongezeko la wagonjwa wapya ingawa wagonjwa wa zamani wameendelea kupata matibabu na kuruhusiwa.

Amesema  Ugonjwa huo unaweza kumalizika ikiwa wananchi watazingatia na kufuata kanuni za usafi ,kula vyakula vilivyotayarishwa katika mazingira safi na salama, matumizi ya maji salama yaliyochemshwa pamoja na kunawa mikono kwa sabuni.

Amesema jitihada zinazofanyika na manispaa hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kupitia magari ya vipaza sauti, kuweka dawa katika madimbwi na mitaro na kutoa dawa za kutibu maji ya kunywa kwa wananchi bure.

Afisa wa manispaa ya Kinondoni Mathias Kapizo amesema wananchi wanatakiwa kubadilika na kuwa makini kutokana na hatari ya maambikizo ya ugonjwa huo ambao mgonjwa akichelewa kufikishwa hospitali hupoteza maisha mara moja.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu wiki iliyopita takriban watu 196 wameugua ugonjwa huo huku 3 tayari wamepoteza maisha.

0 comments: