Wednesday, September 24, 2014

Wednesday, September 24, 2014


Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.


Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat), imemkana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na kueleza kuwa hawahusiki kwa namna yoyote katika mbio zake za urais au kupewa fedha kwa ajili ya kuzigawa kwa Halmashauri Mkuu ya Taifa ya (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wanachama wa Chama hicho.

Katibu Mkuu wa Alat, Habraham Shamumoyo, alisema hayo jana  ijini Dar es Salaam jana, katika mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na habari zilizosambaa kwenye mtandao wa kijamii zenye kichwa cha habari kisemacho ‘Pinda akiuka maadili agawa rushwa kwa Dola za Kimarekani’.

Alisema katika makala hiyo ilielezwa kuwa Pinda anasaidiwa kuratibu zoezi hilo chini ya ofisi ya Alat ukiongozwa na Meya wa Dar es salaam, Didas Masaburi, na kijana mwingine Machumu Munasa kwa kugawa fedha hizo kwa wajumbe wa Nec na CCM ili kujitengenezea mazingira ya mwaka 2015.

Pinda anadaiwa kutangaza nia ya kuwania urais, Agosti 23, mwaka huu katika Ikulu ndogo ya Mwanza jijini Mwanza katika mkutano na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa, madai ambayo hadi leo hajayakanusha.

 “Alat, viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali wamesikitishwa na taarifa hizi za uongo, uzushi, uzandiki na zisizokuwa na hata tone moja la ukweli ndani yake, lengo ni kupotosha umma, kuchafua jina la Alat na Waziri Pinda mbele ya umma wa Watanzania,” alisema.

Shamumoyo alisema Jumuiya hiyo haifungamani na chama chochote au upande wowote wa kisiasa na kwamba wanahusiana na Waziri Mkuu kwa cheo chake na siyo binafsi, hivyo masuala ya urais mwaka 2015 hawahusiani nayo.

Alisema Alat inaundwa na Halmashauri zoye nchini, Manispaa na Majiji na kwamba mkutano mkuu una wenyeviti na Mameya wa halmashauri ambao baadhi yao wanatoka vyama vya upinzani na kwamba Kamati ya Utendaji wajumbe wengi ni kutoka CCM, lakini kuna wajumbe kutoka upinzani.

“Jumuiya ina mfumo wake wa kisiasa na kiutendaji na inaendeshwa kwa kufuata taratibu za fedha ambapo kila mwaka mahesabu yake hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  (CAG) na haijawahi kupokea fedha za Kitanzania, Dola kutoka kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kampeni au kugawa kwa mtu yeyote…inaendeshwa kwa michango halali ya wanachama wake,” alisema.

Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa wakati makala hiyo inaandikwa, Mwenyekiti wa Alat, hakuwapo na kuwa hadi sasa yupo Ujerumani kwa ziara ya kikazi huku akiwataka wananchi kuzipuuza taarifa hizo zisizo na lengo jema kwa Jumuiya hiyo.

0 comments: