Tuesday, September 23, 2014

Tuesday, September 23, 2014

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL), kupitia mradi wa EABL Foundation, mwaka huu tena imetoa ufadhili wa masomo ya chuo kikuu kwa kugharamia kwa asilimia 100 ikiwemo karo, malazi na fedha ya kujikimu kwa mwezi.
Mwaka huu, mradi utatoa ufadhili kwa masomo ya michepuo ya shahada ya biashara, uhandisi, sayansi ya chakula, teknolojia ya mawasiliano na kompyuta kwa wanafunzi ambao wamefaulu kidato cha sita na hawana uwezo wa kujilipia.
Meneja Mradi Endelevu, Hawa Ladha, alisema ufadhili huo ambao hufanyika mara moja kwa mwaka ni kwa watanazania wanaotaka kusoma vyuo vya hapa nchini.
“Wanafunzi waliokidhi vigezo vyote vya kuomba ufadhili huo, watawezeshwa kusoma na kufanikiwa katika malengo yao,” alisema.
Meneja huyo, aliongeza kuwa ufadhili huo wa kipekee ni kwa wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia na akawashauri vijana kuchangamkia fursa hizo, kwani muda wa kuomba haujaisha.
“Fomu za ufadhili zinapatikana katika tovuti ya www.eablfoundation.com na zimebaki siku kumi tu. Maombi hayo ni lazima yambatanishwe na barua ya wito ikionesha mojawapo ya michepuo anaotaka kusoma,” alisema na kuongeza.
Pia awe na uthibitisho wa kuonyesha muombaji hana uwezo wa kifedha kwa ajili ya masomo, kuwasilisha nakala ya cheti cha kumaliza elimu ya  kidato cha sita na cha nne na fomu ya maombi iliyojazwa barua ya kukubaliwa masomo ya chuo kikuu.
Alifafanua kuwa, wanafunzi ambao hawajapata barua za kujiunga  chuo kikuu lakini wana sifa za kujiunga, wanaruhusiwa kuomba.
Mradi wa EABL Foundation ulianza ufadhili kwa wanafunzi wa chuo tangu mwaka 2005 na waliomaliza wako zaidi ya 200 Afrika Mashariki, Tanzania ikiwa na zaidi ya 26 na wanafanya kazi katika kampuni mbalimbali.

0 comments: