Dodoma. Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira amesema hana sababu
ya kuona haya kutangaza kuutaka urais kwa kuwa urais si ukwe ila
anasubiri wakati mwafaka.
Wasira alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini Dodoma.
“Watakaposema ruksa, nitasema na wala kugombea
urais si suala la kuonea haya. Ni kutoa huduma kwa Watanzania. Unalionea
haya la nini? Kwani kugombea urais ni ukwe?” alihoji Wasira na
kuendelea;
“Urais ni mama mkwe wako, hapana. Wakati ukifika
nitasema tu. Na mradi kuna wananchi wanasemasema na wananitia moyo,
ukifika wakati nitasema.”
Hata hivyo, waziri huyo ameonya kuwa endapo urais
utachezewa kwa kuingia mtu ambaye si mwadilifu, biashara atakayoifanya
Ikulu itakuwa ni kuuza haki za watu.
Alisema hawezi kufahamu nani atashinda katika
kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, lakini lazima
rais awe mtu mwenye sifa za kushika nafasi hiyo.
“Mimi siwezi kufahamu ni nani ataongoza Tanzania,
lakini ninaweza kusema sifa.” Alisema Wassira na kutaja sifa hizo kuwa
ni pamoja na kuwa Mtanzania kwa sababu haiwezekani kuagiza mtu kutoka
nje ya nchi kuja kuwania nafasi hiyo.
Aliongeza; “Rais pia anatakiwa kuwa mzalendo
anayeipenda nchi yake na adhihirishe mapenzi yake, awe na uwezo wa
kuongoza na pia ame-prove (amedhihirisha) uwezo wake huo wa kuongoza.”
Sifa nyingine ya urais, aliitaja kuwa ni mgombea
kuwa mtu aliyewahi kuongoza taasisi nyingine na kuwaridhisha Watanzania
kuwa aliongoza vizuri.
“Lakini pia rais lazima awe mwadilifu maana
unalinda haki za watu. Baba wa Taifa aliwahi kusema Ikulu kuna biashara
gani, lakini kuna biashara ya nguvu tu. Unaweza kuuza haki za hao watu,”
alisema na kuongeza;
“Maana chakuuza pale hakuna. Mimi nafanya pale.
Mimi naona watu wanamwagilia maua tu lakini kuna power (nguvu), kama
wewe unapenda hela zaidi kuliko watu waliokuweka pale basi wewe utakuwa
kazi yako ni kuuza haki zao.”
Alisema sifa hizo ni za msingi na wala si ngumu na kama mtu hana, hana tu.
0 comments:
Post a Comment