Sunday, August 30, 2015

Sunday, August 30, 2015
  

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kitajenga viwanda viwili kwa ajili ya kusindika mafuta ya alizeti na pamba katika mkoa wa Singida, kama kitapata ridhaa ya watanzania kuendelea kushika dola.

Mbali na viwanda, serikali ijayo ya CCM pia itajenga hospitali mkoani humo yenye ukubwa kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili itakayokuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa wananchi wa Kanda ya Kati na mikoa ya jirani.

Ahadi hiyo ilitolewa jana na mgombea mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan (pichani kulia) wakati akizungumza na wananchi wa Iramba Magharibi waliojitokeza katika kijiji cha Kyengege. Samia alisema kila kiwanda kitaajiri zaidi ya vijana 600 hivyo kutoa fursa ya ajira kwa vijana.

Iramba Magharibi ni ngome ya mgombea kiti cha ubunge kwa tiketi ya CCM, Mwigulu Nchemba. Samia alisema hatua za awali za mradi huo wa ujenzi wa hospitali zimekwishaanza katika mkoa huo.

Akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa idadi kubwa kuipigia CCM kura, Samia alisema hiyo ndio itakuwa njia pekee ya kumpa fursa ya kutekeleza ilani ya CCM mkoani humo.

Akimzungumzia mgombea ubunge wa CCM katika jimbo hilo la Iramba Magharibi, Samia aliomba wapigakura walioandikishwa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi na kupiga kura kwenye vituo husika.

“Nina uhakika wote waliojiandikisha kupiga kuwa mtaipigia kura CCM na yeyote atakayepiga kura upande mwingine, ngoja niwaambie mtakuwa mmepoteza kura zenu,” alisisitiza.

Aliongeza: “Hakikisheni mnakamilisha majukumu yenu ya kila siku mapema na muache siku ya kupiga kura kwa ajili ya kufanya kazi hiyo moja. “ Mapema mgombea huyo wa Urais kwa tiketi ya CCM alifanya mkutano wa kampeni Singida Vijijini, kata ya Msange ambayo mgombea ubunge katika jimbo hilo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

Akiwa Singida vijijini, Samia aliahidi kushughulikia matatizo ya maji na kuwezesha upatikanaji dawa mahospitalini, kwenye vituo vya afya na zahanati pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa. Alisema Mfuko wa Taifa wa Maji utakaoanzishwa utaongeza nguvu katika juhudi za kupeleka maji vijijini na kukabiliana na matatizo ya maji.

Alisema serikali yake itajenga mabweni kwa ajili ya shule za sekondari, hasa kwa ajili ya wasichana ili kuwalinda dhidi ya wanaume wanaonyemelea mabinti wadogo na kuwasababishia mimba za utotoni.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Singida Vijijini, Nyalandu alisema jimbo lake limekuwa na maendeleo makubwa chini ya chama tawala. Alisema visima vya maji vimeongezeka kutoka 14 hadi 100 chini ya miradi ya maji inayotekelezwa na CCM, zahanati pia zimeongezeka hadi kufikia 40 kutoka 14.

Katika elimu, Nyalandu alisema kulikuwa na shule mbili tu za sekondari wakati anaingia madarakani lakini sasa kuna shule za sekondari 28. Nyalandu alisema jimbo jirani lililo mikononi mwa mpinzani lina maendeleo kidogo na kuongeza kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu mkoa wote wa Singida utakuwa mikononi mwa CCM.

Mgombea mwenza huyo wa Urais, leo ataanza kampeni zake mkoani Dodoma.

0 comments: