Wednesday, September 30, 2015

Wednesday, September 30, 2015
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli (pichani kulia) amesema kuwa wanaokejeli safari za nje za Rais Jakaya Kikwete wapuuzwe.

Dk. Magufuli aliyasema hayo jana katika Jimbo la Mtera Wilaya ya Chamwino, Mvumi mission mkoani Dodoma wakati akizungumza kwenye kampeni za kuomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo.
“Huwezi kujifungia ndani kama fisi halafu utake maendeleo, kwani hata ukiwa na mke ukawa unashinda ndani, lazima akuulize huna marafiki wa kuwatembelea,” alisema.
Aliongeza kuwa, safari ya Rais Kikwete ya hivi karibuni nchini Marekani imefanikisha kupatikana kwa dola za Marekani bilioni 992 sawa na sh. trilioni moja.


Alisema fedha hizo zimetolewa na mradi wa Changamoto za Milenium (MCC), ambazo zitasaidia kuleta maendeleo kwa taifa na katika kusambaza miundombinu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini na mambo mengine.


Dk. Magufuli aliongeza kuwa pindi atakapochaguliwa kuwa rais wa Tanzania wa awamu ya tano, atajivunia kuwa na wazee ndani ya chama chake, hali itakayosaidia kufuata ushauri wa kufanikisha taifa kufikia mafanikio.


Alisisitiza, katika kampeni zake anaahidi vitu vinavyotekelezeka, hali inayowafanya wapinzani kuchomwa na maneno yake kutokana na kueleza ukweli kwa ajili ya mafanikio ya Watanzania.


Akiwa katika jimbo hilo, Waziri Mkuu wa mstaafu, John Malecela alisema wagombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hawana macho kwa kusema kuwa, Serikali ya CCM tangu uhuru haijafanya lolote.


Aliongeza kuwa, Serikali ya CCM imefanya mengi ambayo ni mfano wa kuigwa kwao, ikiwemo ujenzi wa barabara ambazo zinapitika hata na wapinzani.
“Nawaomba Watanzania wote mwaka huu watupeni chini wapinzani na muwape CCM ili iendelee kuwepo madarakani izidi kuleta maendeleo zaidi,” alisema Malecela.


Pia, aliwakumbusha wana CCM kuwa siku zilizobaki kwa ajili ya uchaguzi mkuu si nyingi hivyo wanatakiwa kujipanga vema kwa wajumbe wa nyumba 10 ili kuhakikisha chama kinapata ushindi mnono.


Aliongeza kuwa, ipo ishara kuwa utaratibu wa kupata kura kupitia kwa wajumbe hao siku hizi hautumiki vizuri, hivyo aliwasisitiza kujipanga vema kupitia wajumbe hao kufanikisha ushindi.


Wakati huo huo, mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo hilo, Livistone Lusinde ‘Kibajaji’ alikishukia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa katika mwaka ambao wamepotea, ni mwaka huu.


Alisema kuwa watu waliokichafua ni mafisadi na kuzunguka nchini nzima kutangaza hivyo, ili wasikubalike na Watanzania, leo wamewakumbatia.
Katika mwaka ambao Chadema wamebugi ni mwaka huu, kwani walikuwa wa kwanza kusema Lowassa (Edward), ni fisadi na mgonjwa, lakini leo ndiyo wamemchukua na kumpa nafasi.


Aliongeza kuwa, kwa sasa Watanzania wanahitaji rais msafi na mwenye msimamo kama Dk. Magufuli na kuwaomba Watanzania Oktoba 25, mwaka huu wasifanye makosa kwa kuwachagua wapinzani.


Dk. Magufuli kabla ya kufika katika jimbo hilo alifanya mikutano miwili katika Jimbo la Isimani mkoani Iringa, linalotetewa na mbunge anayemaliza muda wake, William Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.


Baada hapo, akafanya mkutano mwingine katika Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma na kuwaomba wananchi wa eneo hilo kumchagua ili awe rais na mbunge wamchague George Simbachawene na madiwani wa CCM ili kuharakisha maendeleo na baadaye Jimbo la Mtera.

0 comments: