Wednesday, September 2, 2015

Wednesday, September 02, 2015


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu (pichani kulia), Damian Lubuva akizungumza na wanahabari.

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekubali rufani 13 zilizokatwa na wagombea ubunge katika majimbo mbalimbali nchini, huku majimbo 10 ambayo wagombea wake walipita bila kupingwa, imewarejesha.
Kurudishwa kwao kunafanya baadhi ya wabunge waliokuwa wamepita bila kupingwa, sasa kuwa na wapinzani wao na baadhi ya majimbo hayo ni Bumbuli (January Makamba), Peramiho (Jenista Mhagama), Ludewa (Deo Filikunjombe) na Madaba (Mhagama), walitangazwa kupita bila kupingwa.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey wakati akitoa ufafanuzi wa pingamizi za wagombea ubunge na udiwani, yaliyowasilishwa kwenye tume hiyo.
Akizungumzia mapingamizi ya wabunge, Kasilima alisema walipokea pingamizi 56 za wabunge wa majimbo mbalimbali na kati ya hayo, 32 yametolewa uamuzi, huku wagombea 13 wakishinda rufaa hizo.
Majimbo hayo na wagombea waliorudishwa ni kama inavyoonekana kwenye mabano, Jimbo la Kinondoni, rufani mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo, Karama Suleiman aliyewekewa pingamizi na mgombea wa CCM, Idd Azzan imekataliwa na mgombea huyo amerudishwa kwenye kinyang’anyiro.
Wengine waliorudishwa kwenye kinyang’anyiro ni Mwingira Erasmo wa Chadema (Peramiho), Chagola Sechonge-CUF (Mlalo), Daudi Lusewa –Chadema (Mji wa Handeni ) na Shoo Aikaeli –ACT Wazalendo (Chalinze).
Pia wamo Bidyanguze William Ada-Tadea (Kigoma Kusini), David Chamyegh –Chadema (Bumbuli), Msambichako Mkinga –Chadema (Ludewa), Busara Kaisari-ACT Wazalendo (Madaba) na Omari Rashid –CCM (Tanga Mjini).
Waliokataliwa rufani zao ni wagombea wa Jimbo la Rungwe, Frank Magoba wa ACT Wazalendo, Barwany Khalfan wa CUF (Lindi Mjini), Emmanuel Masonga wa Chadema (Njombe Kusini), Khamis Omar (CCM Micheweni) na Michael Joseph ACT Wazalendo (Kasuli Mjini).
Wengine ni Kilewo John –Chadema (Mwanga), Ester Matiko wa Chadema (Tarime Mjini), Celina Kombani wa CCM (Ulanga), Mezza John wa CUF (Nzega Mjini), Bagachwa Abubakar wa CUF (Nkenge), Elias Michael Machibya wa CCM (Bukene), Janeth Mbene wa CCM (Ileje).
Rufani nyingine zilizokataliwa ni za Benson Kigaila wa Chadema (Dodoma Mjini), Seleman Mtutula wa UPDP (Mtama), Jerry Silaa wa CCM (Ukonga), Tumaini Kabusinja wa NCCR-Mageuzi (Sengerema) na Kireti Isaac wa SAU (Moshi Mjini).
Kwa upande wa madiwani, Kailima alisema walipokea pingamizi 200 na kwamba jana walifanyia kazi 54, na kwamba kesho wanategemea rufani zote za ubunge na udiwani ziwe zimeshatolewa uamuzi.

0 comments: