Chama
cha APPT- Maendeleo, kimepongeza kupitishwa kwa Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa katika hatua ya Bunge Maalum la Katiba na kuahidi
kupigania suala la mbunge kuwajibishwa na wananchi liingizwe katika
katiba anaposhindwa kutekeleza majukumu yake badala ya kusubiri miaka
mitano.
Katibu Mwenezi wa Taifa wa chama hicho, Godfrey Davis, akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema APPT- Maendeleo
kimechukua hatua ya kupongeza Rasimu hiyo kwasababu mambo mengi
yanayohusu wananchi na wanasiasa yameingizwa katika katiba hiyo.
“APPT Maendeleo tangu awali tulitoa mapendekezo kwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kwamba Rais ili aweze kutangazwa mshindi apate zaidi ya
asilimia 50, mgombea binafsi awepo, Tume Huru ya Uchaguzi na suala la
matokeo ya Rais yahojiwe mahakamani, yote haya yameingizwa kwenye Rasimu
ya Katiba.
Hivyo tuna sababu ya kupongeza hatua hii,” alisema.Davis alisema
wanasiasa na wadau wengine wanaopinga Rasimu ya Katiba hiyo watambue
kuwa hiyo siyo ya mwisho kwani kutakuwa na kipindi cha mpito mambo
mengine ambayo hayajaingizwa yataingizwa siku za mbeleni.
Alisema pamoja na kupitishwa mambo mazuri katika Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa, APPT- Maendeleo kitaendelea kupigania suala la wananchi
kuwa na mamlaka ya kuwajibisha wabunge wao ili kuleta uwajibikaji
mzuri.
Katibu Mwenezi huyo alisema kuingizwa kwa kipengele hicho katika katiba
kutasaidia wabunge kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao ya
kuwaletea maendeleo wananchi badala ya hivi sasa ambapo baadhi ya
wabunge wamekuwa wakiwatelekeza wapiga kura wao kwa muda mrefu na
kuonekana wakati wa uchaguzi mkuu tu.
Aliongeza kuwa mambo mengine ambayo chama hicho kitaendelea kupigania ni
suala la mawaziri kutotokana na wabunge, mgombea ubunge awe na elimu
kuanzia kidato cha nne, Bunge liwe na chemba mbili yaani wabunge wa
Tanzania na wabunge wa Tanzania bara.
Davis ameiomba serikali nakala za rasimu ya mwisho zitolewe nyingi na
kwa wakati ili wananchi wapate fursa ya kuisoma na kutoa mawazo yao
kabla ya kuchukua uamuzi wa kupiga kura ya maoni.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment