Sunday, October 26, 2014

Sunday, October 26, 2014

Askari wawili wakamatwa katika mikutano ya CHADEMA


CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewabaini na kuwakamata polisi wawili waliokuwa kwenye mkutano wao wilayani Geita wakiwa wamevaa sare za chama hicho huku wakiwa na kadi za uanachama wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake CHADEMA, (Bawacha), Kunti Yusuph alisema, askari hao wa kike na wa kiume walikamatwa na walinzi wa chama hicho (Red Brigedi) ambapo walinyang’anya simu zao za za kiganjani, vinasa sauti na kadi ya CHADEMA.
Yusuph alisema kuwa tukio hilo limeuthibitishia umma namna polisi wanavyotumika kufanya vurugu kwenye mikutano yao ikiwemo tukio la utupaji wa mabomu kwenye mkutano ya chama hicho iliyotokea jijini Arusha Juni mwaka jana  na kusababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa vibaya.
Alisema kuwa wanamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu kuwafukuza kazi askari hao kutokana na kukiuka maadili ya kazi yao inayowakataza kujihusisha na shughuli za siasa.
Alisema kuwa tangu wakiwa jijini Mwanza walipata taarifa za kiintelijensia kuwa kuna njama za viongozi wao kushambuliwa hatua iliyolazimu vijana wa ulinzi wa chama hicho kujipanga barabara na kufanikiwa kuwakamata polisi hao kabla hawajatimiza azma yao.
“Huyo askari polisi wa kike alikamatwa wakati akiwasiliana kwa simu na mtu akimweleza kuwa Halima Mdee yupo ila bado hajapanda jukwaani ambapo  alipopekuliwa alikutwa na kinasa sauti na walinzi wetu wakamnasa na huyo polisi wa kiume akiwa amevalia sare za CHADEMA na akatuonyesha kadi yetu akidai yeye ni kamanda,” alisema.
Alionyesha kadi ya CHADEMA waliyomkuta nayo polisi, Ernest Silayo yenye namba 2151260 ikiwa na picha yake ambayo alikabidhiwa  Oktoba 3,  mwaka huu na katibu wa Bavicha, Gabriel Nyasunga kwenye ofisi za chama hicho wilaya ya Geita ambayo imelipiwa mpaka Oktoba 2015.
“Tulipowakamata wakahojiwa wakatoa maelezo yasiyoeleweka, tuliamua kuwapeleka polisi lakini Mkuu wa Upelelezi ‘OC CID’ akampigia simu mwenyekiti wetu wa Mkoa Alfonce Mawazo akimuomba tuwarudishie kinasa sauti kwa kuwa wale ni polisi na akaomba msamaha kwa yaliyotokea,” alisema
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA alisema kuwa kwa tukio hilo linaendelea kuuthibitishia umma wa Watanzania kuwa polisi walihusika na ulipuaji wa mikutano ya chama.
Juhudi za kumpata kamanda wa polisi mkoani hapa, Joseph Konyo kuzungumzia sakata hilo hazikufanikiwa kutokana na kuwa nje ya ofisi kikazi huku namba yake ya simu ya kiganjani ikiwa imezimwa.

CHANZO:Tanzania Daima

0 comments: