BAADHI ya madereva wa Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), jana waligoma kufanya kazi kwa muda wakipinga agizo la kupeleka hesabu ya sh. 205,000 wakidai kuwa haziwezi kupatikana kutokana na ushindani wa kibiashara.
Mmoja wa viongozi wa madereva hao wa kituo cha Mbagala, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema wanautaka uongozi wa UDA kusikia kilio chao, kinyume chake wataendelea kuvutana kila mara.
Alisema hesabu hiyo haiwezi kupatikana baada ya kampuni hiyo kuingia makubaliano na Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu na Majini (Sumatra), ambako baadhi magari hivi sasa yamepigwa mkanda kuonyesha yanakokwenda, kitendo kinachowazuia kupita njia yoyote kama ilivyokuwa awali.
“Hata hivyo baada ya kugoma, walifika baadhi ya viongozi na kutushauri tukafanye kazi kwa makubaliano kuwa kwa siku ya leo tupeleke sh 130,000 kwa sababu tulichelewa kuanza kazi…tena tukienda njia yoyote ambako hata tungekamatwa kampuni ingehusika yenyewe,” alisema dereva huyo.
Akizungumzia mshahara, dereva huyo alisema wanaitaka kampuni hiyo iongeze mshahara kutoka sh 150,000 hadi 350,000 kwani unaolipwa sasa haukidhi mahitaji.
“Mshahara tunaolipwa hautoshi, hata hivyo haulipwi kwa wakati kitendo ambacho ni kawaida kila mwezi,” alisema.
Aliongeza kuwa waliahidiwa na kiongozi huyo ambaye walishindwa kupata jina lake kuwa madai yao yatashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi ndani ya miezi miwili.
Alipotafutwa Msemaji wa Kampuni hiyo, George Maziku ili kutoa ufafanuzi, alisema kuhusu makubaliano ya Sumatra na UDA hayaathiri chochote kuhusu hesabu hiyo.
Alisema viwango hivyo hawakuviweka tu wakiwa mezani, bali vilifanyiwa utafiti na wataalamu wa kampuni na kubaini kuwa ni sahihi na kinapatikana.
Maziku, alisema suala la kupunguza kiwango hicho wasahau, kwa sababu hesabu hiyo inapatikana kutokana na utafiti wa kampuni na kwamba wanapata fedha nyingi zaidi ya hizo kwa siku.
Kuhusu kuchelewa mshahara, Maziku alisema kuwa suala hilo lilichangiwa na mifumo ya kibenki hata hivyo hivi sasa limekwisha.
0 comments:
Post a Comment