Monday, October 20, 2014

Monday, October 20, 2014


Makamu wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dk. Mohammed Gharib Bilal amesema kamwe serikali haitaruhusu mtu yeyote au kikundi cha watu kuchezea amani iliyopo nchini, kwani amani ya Tanzania ni lulu inayoliliwa na watu wa mataifa mengine hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuilinda na kuitunza kwa nguvu zote.

Dk. Bilal ameyasema hayo wakati wa sherehe ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kazini kwa askofu mteule wa kanisa la African Inland Church dayosisi ya Mwanza, Baba askofu John Binango Mditi, sherehe iliyofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kuhudhuriwa na maelfu ya waumini wa kanisa hilo, wachungaji na baadhi ya maaskofu kutoka makanisa mbalimbali nchini, wakiongozwa na askofu mkuu wa kanisa hilo hapa nchini askofu Silas Kezakubi.

Akihubiri wakati wa ibada hiyo ya kumweka wakfu na kusimikwa kazini kwa askofu mteule John Bunango, askofu mkuu wa kanisa la African Inland Church Tanzania ambaye pia ni askofu wa dayosisi ya Tabora Silas Kezakubi amewaasa vijana kutokubali kutumiwa na baadhi ya watu kuvuruga amani badala yake watumie nguvu za msuli walizonazo katika kupambana na adui umaskini.

Akizungumza mara baada ya kuwekwa wakfu, askofu John Bunango Mditi ambaye anakuwa askofu wa tatu wa dayosisi ya Mwanza, baada ya askofu Daniel Nungwana ambaye amestaafu baada ya kuhudumu katika dayosisi hiyo kwa miaka 13, ameiomba serikali kulinda usalama wa maisha ya viongozi wa dini kutokana na matukio yaliyojitokeza katika siku za hivi karibuni ya baadhi ya viongozi wa dini nchini kushambuliwa, kujeruhiwa na hata kuuawa.

Kanisa la African Inland Church dayosisiya Mwanza lilianzishwa miaka 21 iliyopita. Kanisa hilo hapa nchini hivi sasa linakadiriwa kuwa na waumini wanaofikia milioni moja na jumla ya makanisa 2,069 kote nchini, kanisa hilo pia limekuwa chachu ya injili kwa mataifa mengine kwa kupanua huduma zake nje ya mipaka ya tanzania ikiwemo kuanzisha kanisa hilo katika nchi ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Burundi na Msumbiji.

0 comments: