Mwanamke anyeshukiwa kuwa na Ebola akilia nje ya zahanati Sierra Leo

Mwanamke anayeshukiwa ana Ebola akilia nje ya zahanati Sierra Leone.

Rais wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma, ameteua tume mpya ya kupambana na ugonjwa wa Ebola ambao umeuwa watu 1,200 nchini humo.
Tume hiyo mpya itasimamiwa na waziri wa ulinzi, Meja Alfred Palo Conteh, na itaripoti moja-kwa-moja kwa Rais Koroma.
Taarifa ya rais ilieleza kuwa alilazimika kufanya mabadiliko hayo kwa sababu ya kazi kubwa ilioko ya kupambana na Ebola nchini Sierra Leone.
Umoja wa Mataifa umeanza kusambaza chakula katika mji mkuu, Freetown, kwa sababu watu wengi wanaogopa kutoka nje ya majumba yao wasije wakaambukizwa ugonjwa huo.
Na Rais Obama ameonya watu wasiingiwe na taharuki kubwa kuhusu ugonjwa wa ebola na alisema kuwa Marekani haitazuia safari za ndege kutoka nchi za Afrika Magharibi zilizoathirika na ugonjwa huo.
Rais Obama alisema hatua kama hiyo itafanya hali kuzidi kuwa mbaya.
Taarifa hiyo imetoka wakati vyombo vya habari vya Marekani vinaarifu kuwa Bwana Obama, faraghani, ameonesha hasira jinsi serikali yake ilivvyoshughulikia msukosuko huo wa Ebola.
Ijumaa, mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, David Nabarro, alitetea juhudi zilizofanywa kimataifa kupambana na ugonjwa huo.
Bwana Nabbaro alikuwa akijibu lawama za shirika la madaktari wasio na mipaka, MSF, kuwa ahadi za kimataifa za matibabu na msaada, bado hazikupunguza mfumko wa ugonjwa wa Ebola.