Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande
Jaji Mkuu, Mohammed Othman Chande, amekumbusha umuhimu wa kuboresha au kufuta sheria kandamizi 40 zilizotajwa na Tume ya Jaji Nyalali ili kutenda haki kwa jamii na kusimamia utawala wa sheria.
Jaji Mkuu, Mohammed Othman Chande, amekumbusha umuhimu wa kuboresha au kufuta sheria kandamizi 40 zilizotajwa na Tume ya Jaji Nyalali ili kutenda haki kwa jamii na kusimamia utawala wa sheria.
Akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), uliofanyika huku wakiadhimisha miaka 60 ya chama hicho jijini hapa juzi, Jaji Mkuu Chande, chama hicho kwa kushirikiana na Tume ya Kurekebisha Sheria nchini (LRCT), zisaidie kuona namna ya kuziboresha.
Alisema utoaji wa haki na utawala wa sheria ni masuala ambayo hayawezi kutenganishwa, hivyo ni wakati muafaka kwa taasisi husika kuzifanyia marekebisho sheria zinazokandamiza haki na utawala wa sheria.
Hata hivyo, alisema, baadhi ya sheria kandamizi tayari zimeshafanyiwa kazi, na akataka TLS pamoja na LRCT kuwa tayari kusaidia sheria zingine zilizobaki.
“TLS ipo tayari kusaidia sheria zingine, na Tume nayo itoe kipaumbele zaidi sheria hizi ziboreshwe,” alisema.
Lakini alisema mwenye jukumu la kuwasilisha bungeni maboresho au muswada wa kuzifuta ni Mwanasheria Mkuu.
Tume ya Jaji Nyalali (1992) iliyokusanya maoni kuhusu namna ya kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ilipendekeza kufutwa kwa sheria 40 kandamizi, ikiwamo Sheria ya Magazeti namba 3, ya mwaka 1976.
Kwa upande wake, Mhadhiri mwandamizi na Mkuu wa Shule ya Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamaganda Kabudi, pamoja na kuipongeza TLS, alipendekeza matumizi ya Kiswahili katika utoaji wa haki mahakamani.
Alitaka Kiswahili kitumike katika mahakama za juu pia lakini changamoto ipo kwenye istilahi zake. “Lugha hii ni yetu na siyo ya kuazima, hivyo lazima tukienzi…wakati umefika sasa kuanza kutumia Kiswahili, lakini lazima tuwe na istilahi zake,” alisema na kuongeza kutumia Kiswahili hakumaanishi kwamba hatujui Kiingereza.
Katika mkutano huo, Jaji Mkuu Chande alizindua tovuti ya TLS.
0 comments:
Post a Comment