Sunday, February 22, 2015

Sunday, February 22, 2015

Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (pichani), amesema anaweza asigombee ubunge kwenye uchaguzi mkuu ujao.


Ndesamburo (80), ameliongoza jimbo hilo kwa vipindi vitatu, tangu mwaka 2000, 2005 na 2010.
“Nitatangaza wakati ukifika kama nitagombea au sitagombea. Naapa mbele yenu kwamba, nitatumia malipo yangu yote yanayotokana na kiinua mgongo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania; zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya kumuunga mkono, yeyote atakayechaguliwa na chama changu, kupeperusha bendera ya Chadema,” alisema Ndesamburo.
Aliyasema hayo jana, wakati akifungua semina elekezi ya siku moja kwa viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na viongozi wapya wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Manispaa ya Moshi. Aliwataka wakazi wa Moshi pamoja na wakereketwa wanaoamini na kutetea siasa za mabadiliko, waendelee kuamini jimbo hilo, atalitetea kwa nguvu zake zote, hata kama atang’atuka madarakani baada ya muda wa ubunge kukoma kikatiba; kwa kuwa hata wapinzani wao CCM, wanazifahamu nguvu zake katika siasa, na kubatizwa jina la ‘Ndesa Pesa’.
Hata hivyo, kumekuwapo na minong’ono ndani ya chama hicho, kwamba miongoni mwa wanachama wa Chadema; wanaotajwa kumrithi Ndesamburo katika kiti chake cha ubunge kuwa ni Meya wa sasa wa Manispaa ya Moshi, Japhary Michael.
Ndesamburo aliwaasa wanawake hao kuvunja makundi waliyotoka nayo katika uchaguzi uliofanyika ndani ya chama na kuungana ili kuisaidia Chadema kutwaa viti vyote vya udiwani na ubunge Manispaa ya Moshi.
“Mkiendelea na makundi, mtawapa CCM nafasi ya kushinda lakini kama mnataka tuendelee kuwatesa kwenye ubunge na udiwani; vunjeni makundi yenu ili tuendelee kuongoza halmashauri tuliyonayo. 
Hamshangai Rais, Jakaya Kikwete alikuja Moshi na kuisifia Halmashauri inayoongozwa na Chadema…Ameikubali kazi ya Meya (Japhary Michael) na madiwani wake, wakisaidiwa na mbunge,”alisisitiza.
Ndesambauro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, aliwasisitiza viongozi hao wa Bawacha, kujipanga vyema kwa kujiwekea mikakati thabiti inayotekelezeka kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, mwaka huu.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) na Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kihwelu, akimshukuru Ndesamburo kwa kuwaunga mkono wanawake, alisema Baraza hilo limefanikiwa kuwaweka pamoja wanachama wake na kuyavunja makundi ya chaguzi.
“Tunakuahidi mheshimiwa Mwenyekiti wa mkoa, kwamba tumejenga umoja na kujiimarisha. Tayari tumeanza kuwaanda viongozi na wanachama wetu kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwa wingi katika daftari la kudumu la wapiga kura, wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itakapoanza rasmi zoezi hilo mkoani hapa,”alisema Grace.
Awali, Katibu wa Bawacha Manispaa ya Moshi, Ovena Kowero, akizungumza katika semina hiyo, alisema hadi kufikia sasa, baraza hilo limefanikiwa kudahili wanachama wapya 1,300 kutoka katika viunga vya mjini huo.

0 comments: