Friday, March 20, 2015

Friday, March 20, 2015



Hatimaye huduma za kijamii zilizosimama kwa siku 14 katika vijiji vitatu vya kata ya Isaka wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga zimerejea baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuwajengea nyumba za muda waathirika waliokuwa wamekusanyika kwenye kambi maalum katika shule ya msingi Makata.
Hatua hiyo imewezesha shule ya msingi Mwakata, ambayo awali ilitumika kuwahifadhi wahanga wa mafuriko hayo kufunguliwa rasmi na kupatiwa misaada ya vifaa vya ujenzi,mahitaji muhimu kwa wanafunzi zikiwemo sare za shule na chakula kutokana na wahisani kuendelea kujitokeza kusaidia jamiii iliyoathirika na mafuriko ya mvua ya mawe.


Mashuleni wanafunzi wameonekana wakiendelea na masomo huku wananchi wa wakirejea kwenye maeneo yao baada ya kujengewa nyumba za muda ambapo mtunza hazina wa kamati ya maafa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Bw.Patrick Kalangwa amesema kuwa  Halmashauri yake imeanzisha zoezi la  uelimishaji kwa jamii namna ya kujenga nyumba bora, kilimo cha umwagiliaji na ufugaji samaki kwa lengo la kuwapunguzia umasikini unaowakabili wananchi kwa wakati huu.
Kufuatia hali hiyo kampuni ya bia Tanzania TBL, imetoa msaada wa saruji mifuko 130 na bati 176 huku shirika la kutetea haki za watoto  la TDH la mjini Kahama likitoa msaada wa sare za shule,viatu,vifaa muhimu vya masomo,chakula,sukari,turubai na vyombo vya kupikia vyenye thamani ya shilingi milioni 70.Akipokea msaada huo,mwalimu mkuu wa shule ya msingi  Mawakata ameshukuru wahisani kwa kuwapatia msaada huo kwa kuwa wanafunzi walio wengi hawana sare za shule wala madaftari.
Hivi karibuni mvua iliyonyesha takribani saa moja ilisababisha vifo vya watu 47, wengine 118 kujeruhiwa, kaya 649 kukosa makazi katika kijiji cha Mwakata,Nhumbi,Magugung’hwa na shule ya msingi Mwakata kufungwa kwa muda kutokana na madhara ya mvua hiyo.

0 comments: