DSCN9207
Mwenyekiti wa Klabu ya Maveteran, Mussa Kisoky (katikati) akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano wao juu ya Bonanza hilo la Maveteran wa Afrika Mashariki litakalofanyika Aprili 4 hadi 5, mwaka huu. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Mtemi Ramadhani  na kwa upande wa kulia ni, Lawarence Mwalusako, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Idara habari MAELEZO, jijini Dar es Salaam.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye michuano ya Bonanza la ‘Veterans’ wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki  litakalofanyika kuanzia Aprili 4 hadi 5, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Bonanza hilo linatarajia kuzikutanisha  timu za Ukanda huu wa Afrika Mashariki, Zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Pamoja na Zanzibar huku  Tanzania Bara yenyewe ikiwa mwenyeji na mwandaaji.
Wakizungumza  na wandishi wa habari jana Machi 4, katika ukumbi wa MAELEZO, Jijini Dar es Salaam, wakati wa utambulisho wa Bonanza hilo,  lenye kauli mbiu ‘Acha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ‘albino’, Mtu mwenye albinizimu ni kama mimi na wewe’.  Litakuwa la kipekee mwaka huu huku watu mbalimbali wakitarajiwa kulishuhudia bure.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Mtemi Ramadhan  alisema kwa sasa tayari nchi tatu Kenya, Rwanda na Burundi zimesha thibitisha ushiriki wao   na  wamesha pelekewa barua ya ushiriki wao huku Nchi ya Uganda na kwa upande wa Zanzibar wakiwa kwenye mazungumzo ya mwisho.
“Bonanza hili litakuwa ni la kipekee ambalo pia litakuwa ni ujirani mwema kwa baina ya wachezaji wa zamani waliotamba kwenye timu za Taifa, vilabu na timu za mashirika ya serikali na watu binafsi kukutana pamoja na kukumbushia enzi katika soka hivyo tunaomba watu kujitokeza kwa wingi hiyo Aprili 4 hadi 5 mwaka huu” alieleza ,Mtemi Ramadhan ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji wa klabu ya Simba ya jijini Dar s Salaam na timu ya Taifa, miaka ya nyuma.
Kwa upande wake, Mussa Kisoky ambaye ni mwenyekiti wa Klabu ya Maveterani hao, alibainisha kuwa, kwa sasa pia tayari wameanza utaratibu wa kuonana na Rais Jakaya Kikwete kuwa mgeni rasmi kwani kwa sasa kwa heshima mbali ya kuwa Rais wa Jamhuri wa Tanzania, pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na pia amekuwa mstari wa mbele katika suala hili la kupambana na mauaji na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi wenye albinizim.
“Rais Jakaya Kikwete tunamtarajia kuwa mgeni rasmi kati ya kufungua ama kufunga Bonanza letu hili. Hivyo kwa sasa tunaendelea na taratibu ya kumshirikisha kwa heshima yake aliyonayo ikiwemo kuona michezo inastawi hapa nchini kwa watu wa rika zote” alisema Mussa Kisoky ambaye pia nikiongozi wa SPUTANZA.
Naye kiongozi wa Klabu za Maveterani hao, Lawrence Mwalusako ambaye aliwahi kuzichezea timu za klabu za Yanga, Pan Africa, Timu ya Taifa na nyininge, aliwataka watanzania kujitokeza kwa wingi katika bonanza hilo kwani litakuwa ni bure kwa watu wote.
Mwalusako alisema kuwa, Bonanza hilo linatarajiwa kufanyika kwa siku mbili yaani Aprili 4 hadi 5, mwaka huu kati ya Uwanja wa Karume uliopo Ilala Jijini Dar es Salam ama ule Shamba la Bibi Uwanja wa zamani.
Suala la wadhamini.  Hata hivyo Maveterani hao wamewataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia Bonanza hilo ikiwemo kuwapatia udhamini. “Hadi sasa tumepanga kutumia kiasi cha zaidi ya sh milioni 25, Ambazo zitasaidia katika kufanikisha shughuli hii ikiwemo maandalizi ya ndani na timu zote kutoka Nje ya Tanzania na uendeshaji…wadau tunawaomba sana kujitokeza kutuunga mkono” alisema Mussa Kisoky ambaye ni mwenyekiti wa maveteran hao.
Hata hivyo, Maveteran hao walibainisha kuwa, tayari wameshapeleka maombi yao ya udhamini kwa watu mbalimbali ikiwemo taasisi na makampuni yaliyopo hapa Nchini ilikuwapiga tafu.
Bonanza hilo limeandaliwa na  Klabu ya Maveteran wa Tanzania ‘TANZANIA STARS’ ambapo wachezaji wa zamani mbalimbali watajumuika katika kusakata kabumbu dhidi ya wachezaji wenzao wa  zamani wa Afrika Mashariki hii itakuwa ni wakati wa siku kuu ya Pasaka.