Tuesday, March 31, 2015

Tuesday, March 31, 2015
unnamed222
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imetangaza ugunduzi wa gesi asilia katika Miamba ya Mchanga kwenye kisima kinachochimbwa na Statoil cha Mdalasini-1 kwenye bahari kuu ya Tanzania.
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. George Simbachawene amebainisha hayo kwenye mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dodoma. Baada ya kuthibitishwa na Makamu wa Rais wa Statoil, Nick Maden pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
“ugunduzi huo wa gesi asilia wa futi za ujazo trilioni 1.0-1.8, unaongeza kiwango cha gesi asilia iliyopatikana kwenye kitalu namba 2 kufikia futi za ujazo trilioni 22. Kisima cha Mdalasini -1 kimechimbwa katika urefu wa mita za maji ya bahari 2,296 kusini mwa kitalu namba 2” alisema Mhe. Simbachawene.
“kuanzia mwanzo wa uchimbaji, Februari 2012, tumechimba visima 13 na tumefanya ugunduzi katika visima 8 ikiwemo Mdalasini-1. Bado tunaona uwezekano wa gesi zaidi katika eneo la Kitalu namba 2” aliongezea Mhe. Simbachawene
Statoil ni Mkandarasi katika Leseni ya Utafutaji ya Kitalu namba 2 kwa niaba ya TPDC na ina hisa ya asilimia 65% na mshirika wake Exxon Mobil and Production Tanzania Limited ina hisa asilimia 35%.
Wakati wa uendeshaji baada ya Serikali kutoa Leseni ya uzalishaji, TPDC kulingana na mkataba inaweza kushiriki katika uendeshaji na uzalishaji kwa kutwaa asilimia 10% ya uwekezaji.

0 comments: