Kileo aliweka pingamizi dhidi ya Waziri wa Maji na mbunge anayemaliza muda wake, Profesa Jumanne Maghembe, (pichani kulia CCM) na Mgombea wa NCCR-Mageuzi, Youngsaviour Msuya.
Kwa mujibu wa Kileo, wagombea hao hawakuwa wamewasilisha tamko rasmi la kisheria lililotolewa mbele ya hakimu mkazi wa Wilaya ya Mwanga na pia, hawakuwa wamedhaminiwa na vyama vyao.
Kileo alidai mihuri iliyogongwa katika fomu zao ni ya katibu wa wilaya badala ya ofisi ya wilaya. Pia, alidai kuwa picha ya Profesa Maghembe haikupigwa ndani ya miezi mitatu.
Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Jamhuri William ametupilia mbali sababu hizo akidai kuwa kumbukumbu alizonazo ofisini kwake wagombea hao wamedhaminiwa na vyama vyao.
Alisema hatua ya Msuya kutoa tamko mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Moshi haimuondolei sifa ya kuteuliwa mgombea na pia, haoni tatizo kwa Profesa Maghembe kula kiapa Mahakama ya Mwanzo. “Masuala yanayohusu mihuri ya chama inategemea na muundo wa uongozi na utendaji katika chama husika. Hakuna kosa kwa katibu wa wilaya kugonga muhuri wake,” alisema msimamizi huyo.
William alifafanua kuwa suala la umri wa picha ya Profesa Maghembe halina uthibitisho na kwamba, malipo ya risiti ya tamko rasmi siyo mojawapo ya sharti la uteuzi wa mgombea ubunge.
Baada ya kutupwa kwa pingamizi lake, Kileo aliliambia gazeti hili jana kuwa atakata rufaa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akipinga uamuzi huo wa msimamizi kuwa haukutenda haki.
Kileo alisema mathalani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka jana, baadhi ya wagombea wa Chadema walienguliwa baada ya fomu zao kugongwa muhuri na katibu wa wilaya.
0 comments:
Post a Comment