Friday, September 11, 2015

Friday, September 11, 2015


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo,Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Bw. Ferrao,(pichani kulia) alisema kuwa ni fahari kubwa kwao kuona msimu mpya wa ligi hiyo unaanza hivyo kutoa fursa kwa wapenzi wa soka nchini na kwingineko kupata burudani.

Alizitaka timu zote pamoja na mchezaji mmoja mmoja, kucheza kwa kufuata sheria zote 17 za soka ili kuutendea haki mchezo huo, lakini pia mashabiki ambao wamekuwa wakimiminika kwa wingi viwanjani kuzishabikia timu zao.

Ferrao aliwaonya viongozi, wachezaji na hata waamuzi kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri matokeo ya mchezo husika, zaidi ikiwa ni rushwa na ushirikina ambao mara nyingi umekuwa ukihusishwa katika kupunguza uhondo wa soka kwa wachezaji kutojituma uwanjani wakiamini ‘ushindi ni lazima’.

“Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inapoanza mwishoni mwa wiki hii, wachezaji wa timu zote shiriki, ni vema wakatambua kuwa Vodacom inawajali ndio maana tumeongeza udhamini kutoka Sh bilioni 1.8 hadi bilioni 2.3  ili kuifanya ligi kuwa na msisimko wa aina yake, lakini pia kuboresha maisha ya wachezaji,” alisema.

Juu ya udhamini wao wa miaka mitatu katika ligi hiyo, Ferrao alisema kuwa wameongeza dau kwa kuwa timu zimeongezeka kutoka 14 msimu uliopita hadi 16 msimu huu, lakini pia wakifanya hivyo ili kuiboresha na kuongeza ushindani miongoni mwa wachezaji na timu kwa ujumla.

Ferrao aliwataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi viwanjani kuzishangilia timu zao ili kuwapandisha mzuka wachezaji waweze kujituma kadri ya uwezo wao na kupata ushindi.

Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa watetezi Yanga, Azam na Simba za Dar es Salaam, Mbeya City na Prisons (Mbeya), Toto Africans (Mwanza), Kagera Sugar (Kagera), Mwadui na Stand United (Shinyanga), Coastal Union, African Sports na Mgambo Shooting (Tanga), Mtibwa Sugar (Morogoro), JKT Ruvu (Pwani), Ndanda FC (Mtwara) na Majimaji (Ruvuma).
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo, kesho Simba itavaana na African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Azam watawakaribisha Prisons (Azam Complex), JKT Ruvu na Majimaji (Majimaji, Songea) na Mgambo watakuwa wageni wa Ndanda (Nangwanda Sijaona).

Mbeya City watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar (Sokoine), Mwadui wataifuata Toto African (Kirumba), Stand Utd wataikaribisha Mtibwa (Kambarage), wakati mechi nyingine itachezwa Jumapili kwa Yanga kuikaribisha Coastal Union (Uwanja wa Taifa).

0 comments: