Thursday, September 10, 2015

Thursday, September 10, 2015
Baadhi ya wasomi na wanaharakati wamekemea kauli ya mgombea urais wa CCM, Dkt. John Magufuli (pichani kulia) ambaye amekuwa akiwaonya wanaotaka mabadiliko ya haraka nchini kwa kuwakumbusha yaliyojitokeza nchini Libya.

Wasomi hao wameiita kauli hiyo ni ya vitisho kwa wananchi, kwani mabadiliko wanayoyataka ni ya kidemokrasia tofauti na nchini Libya ambapo mabadiliko yao yalikuwa ya kivita.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Sikika Nd. Irenei Kiria, amesema wananchi wamejiandaa kwa ajili ya kupiga kura na siyo vita kama wachache wanavyofikiri.

"Mabadiliko yanayozungumzwa na wengi ni ya kidemokrasia na siyo vita, hivyo Dkt. Magufuli hapaswi kutolea mfano wa Libya, tumejiandaa tangu 2010" alisema.

Aliendelea kusema : "Ukweli ni kwamba kuna watu wamekuwa wanataja vita hapa nchini tangu mwaka 1995 hao wanatamani kuleta machafuko wamethubutu kufananisha na Rwanda au Burundi, wakati nchi hii ni tofauti kwani CCM imekuwa madarakani kwa miaka 50 na amani ipo" , alisema Kiria.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bisima amesema wakati wa kampeni si wa kutoa kauli za vitisho badala yake,, wananchi wanachohitaji ni kusikiliza sera za vyama husika ambavyo vitawawezesha kufanya uamuzi wa kuvichagua.

Akiwa kwenye mikoa ya Morogoro na Tanga, Dkt. Magufuli amekuwa akitoa kauli za kuwaonya wanaotaka mabadiliko kuwa wakumbuke yaliyotokea nchini Libya ambapo nchi hiyo imetumbukia kwenye machafuko baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo marehemu Muamar Gadhafi.

0 comments: