Friday, September 26, 2014

Friday, September 26, 2014

Wakili Peter Kibatara na mwanasheria wa Serikali njee ya korti



MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imelitaka Bunge Maalumu la Katiba kuandika na kupitisha vipengele kwa kuzingatia rasimu iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba.

Uamuzi huo uliotolewa jijini Dar es Salaam jana  na jopo la majaji watatu; Augustine Mwarija, Aloysius Mujulizi na Dk. Fauz Twaib waliokuwa wakisikiliza kesi ya kikatiba namba 28 la mwaka 2014  lililofunguliwa na Mwandishi wa Habari, Saed Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo, Kubenea aliyekuwa akiwakilishwa na mawakili, Peter Kibatara na Mabere Marando, anaitaka Mahakama Kuu itoe tafsiri sahihi juu ya mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba, chini ya kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya mwaka 2011.
Akitoa uamuzi huo  chini ya hati ya haraka kwa niaba ya majaji wenzake, Jaji Mwarija alisema mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba yana mipaka, na kwamba madaraka yake yanaongozwa na kutekelezwa kupitia rasimu.

Alisema bunge hilo linaweza kubadili na kuboresha mapendekezo yaliyomo katika rasimu, ilimradi maboresho yasiende kinyume na misingi iliyowekwa na kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kama ilivyokuwa pia kwa Tume.

Jaji Mwarija alisema mahakama hiyo imetoa uamuzi huo  haraka kutokana na unyeti wa suala hilo na kwamba sababu za uamuzi huo zitatolewa Oktoba 7, mwaka huu.Katika uamuzi huo uliosainiwa na majaji hao, mahakama imekiri kuwa kuna mgogoro kati ya tafsiri ya Kiswahili na Kiingereza kuhusu kifungu cha 25 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83.

Licha ya kuwepo mgogoro huo,  Jaji Mwarija alisema baada ya mahakama hiyo kusoma vema tafsiri ya kisheria imetafsiri kuwa Mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maana yake ni uwezo wa kuandika na kupitisha rasimu ya katiba itakayoletwa kwa wananchi wa Tanzania kupigiwa kura.

Mahakama hiyo iliongeza kuwa Mamlaka ya Bunge Maalum ya kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa yatatekelezwa baada ya Rasimu ya Katiba kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume.
Aidha, alisema katika kufanya hayo Bunge Maalumu la Katiba lina uwezo wa kuboresha au kufanya mabadiliko, lakini mamlaka hayo yana mipaka kama ilivyokuwa imeanishiwa katika kazi za tume ya mabadiliko ya katiba kifungu 9, kipengele cha 2 kinachosema kuwa katika kutekeleza masharti ya kifungu kidogo cha (1), Tume itaongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo:
(a) kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano; (b) uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama; (c)mfumo wa kiutawala wa kijamhuri; (d)uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; (e)umoja wa kitaifa, amani na utulivu; (f) uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura;
(g) ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu; (h)utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo washeria; na (i) uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yoyote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.

Aidha katika uamuzi huo, Mahakama imesema kuhusu chanzo cha mabadiliko na ukubwa wa mabadiliko katika rasimu ni suala la kisiasa na wala sio la kisheria, lakini ikasisitiza kuwa mabadiliko yatakayofanyika yasikiuke kifungu cha 9 kipengele cha 2 cha sheria.

0 comments: