Friday, September 26, 2014

Friday, September 26, 2014
BAADHI ya wanasiasa mkoani Rukwa, wametajwa kuwa sehemu ya kikwazo cha kutofanikiwa kwa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwa kile kilichodaiwa kuwakataza wananchi kuchangia gharama.

Mratibu wa CHF Mkoa, Abriel Mkaro, alisema hayo mjini hapa jana alipokuwa akitoa mada katika kikao kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito, sambamba na kuhimiza jamii kujiunga na CHF.Alisema baadhi ya madiwani wamekuwa wakiingilia zoezi la CHF kwa kukataza wananchi wasitoe mchango wa sh 10,000 kwa kisingizo ni gharama kubwa na hawezi kumudu kutokana na kukabiliwa na umasikini wa kipato.

Alisema hali hiyo imesababisha wananchi wengi wasiwe na mwamko wa kujiunga na mfuko huo, hivyo kujikuta wakiendelea kupata matibabu kwa gharama kubwa na wengine wakishindwa kabisa kumudu gharama hizo.

Alishauri wanasiasa kuacha tabia hiyo, kwani uchumi wa wananchi wengi kwa mikoa wa Rukwa na Katavi unawapa fursa ya kujiunga na mfuko huo ambao unawawezesha kupata matibabu kwa gharama nafuu.Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, alitaka kamati za afya za halmashauri za wilaya ziweke usimamizi mzuri wa vifaatiba na dawa zinazofikishwa kwenye zahanati na vituo vya afya, ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, hali ambayo itapunguza kero ya ukosefu wa dawa kwa wananchi.

Takwimu zinaonyesha kimkoa idadi ya kaya zilizojiunga na CHF ni 3,450 kati ya kaya 199,766 sawa na asilimia 1.72 wakati malengo ya kitaifa kufikia 2015 ni asilimia 30.

0 comments: