Wanajeshi wa Nigeria

Kesi imeanza ya askari 59 wa Nigeria kuhusiana na madai kuwa askari hao walikataa kupigana dhidi ya wanamgambo wa kiislam wa Boko Haram .
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutotii amri za kijeshi na kuchangia katika kukaidi amri hizo.
Wote wamekana mashtaka hayo katika kesi iliyosikilizwa katika mji mkuu Abuja.
Wizara ya ulinzi nchini humo inasema hii ni idadi kubwa ya askari kuwahi kushtakiwa nchini Nigeria .
Mwendesha mashtaka asema wanajeshi hao kutoka kikosi maalum kiitwacho Special Forces Batallion,walikataa kutii amri waliokuwa wamepewa kwenda kujumuika na wenzao huko miji ya kaskazini mwa Nigeria ambako jeshi la nchi hiyo linapigana na wanamgambo wa Boko Haram.

Wanamgambo wa Boko Haram wamekuwa wakihangaisha wananchi wa Nigeria
Lakini wakili anaetetea wanajeshi hao walioshtakiwa amesema mwendesha mashtaka hana ushahidi wowote kuhusiana na madai hayo.
Mwezi uliopita kikundi kingine cha wanajeshi waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kumfyatulia risasi na kumuua kamanda wao walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifo.
Kundi hilo linasemekana walipandwa na hasira baada ya wenzao kuvamiwa na wanamgambo hao wa Boko Haram.
Tangu kuzuka mashambulio baina ya serikali ya Nigeria na wanamgambo wa Boko Haram vikosi vya Nigeria vimelalamikia uhaba wa silaha na zana nyenginezo za kupambana na Boko haram na kuwa maslahi yao pia hayashughulikiwi.
Jambo lililopelekea kutokuwepo na moyo wa kujitolea kazini.
Boko Haram wameteka na kuchukua udhibiti miji kadhaa ya kazkazini mashariki mwa nchi hiyo hivyo kuzua maswali kuhusiana na uwezo wa jeshi hilo wa kuilinda nchi hiyo na raia wake.