Friday, October 17, 2014

Friday, October 17, 2014

 Jaji Mstaafu Damian Lubuva
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji mstaafu Damian Lubuva

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inakutana leo kuangalia namna ya kuanza kwa zoezi la uandikishwaji daftari la wapiga kura ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema kwa sasa bado wako katika maandalizi ili kuanza zoezi hilo linalotumia mfumo mpya wa Biometric Voter Registration (BVR).

Alisema kuwa baada ya kumaliza kikao hicho, atakuwa katika nafasi nzuri ya kuuelezea umma utaratibu mzima utakavyokuwa.
“Hivi sasa bado tupo katika maandalizi ya mwisho lakini kesho tunatarajia kukutana katika kikao… hivyo ukinitafuta baada ya kikao nitaweza kukupa tarehe rasmi ya kuanza kwa zoezi hilo la uandikishwaji,” alisema.

Jaji Lubuva, aliwataka wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya mfumo huo kwa kuwa utakamilika mapema kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Alisema pamoja na Mwanasheria Mkuu (AG), Fredrick Werema, kutarajia kutoa msimamo wa serikali juu ya kura ya maoni, NEC yenyewe itaendelea na zoezi hilo kama ilivyopangwa.
“Nadhani tumeona Werema jana alivyosema, hivyo sisi tutaendelea na taratibu na baada ya kikao cha leo tutaweka wazi ni siku gani zoezi hilo litaanza rasmi,” alisema.
BVR ni mfumo mpya ambao unaanza kutumika hapa nchini, licha ya Zanzibar kuutumia tangu mwaka 2009.

Baadhi ya wanasiasa wameonyesha wasiwasi kutokana na NEC kuanzisha mfumo huo ambao ulitangazwa kuanza Septemba mwaka huu.
Wanasiasa hao, walisema kuwa mfumo huo umetambulishwa kipindi kifupi wakati kuna changamoto zake.

CHANZO: Tanzania Daima.

0 comments: