Taarifa
kutoka Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, zinasema kuwa idadi kubwa ya
wanawake wengine wametekwa nyara na kundi la wapiganaji la Boko Haram.
Wiki jana maafisa wakuu wa nchi hiyo walitangaza kufikia makubaliano ya kusitisha vita na kundi hilo.Kwa hiyo kundi hilo lilikubali kuwaachilia wasichana zaidi ya mia mbili waliotekwa na kundi hilo kama sehemu ya makubaliano hayo miezi sita iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo, wapiganaji wa Boko Haram walishambulia vijiji viwili katika jimbo la Adamawa - Waga Mangoro na Garta.
Kisha wakawateka wasichana na wanawake wengi.
Vijiji hivi vinapakana na miji ya Madagali na Michika ambayo imekuwa chini ya udhibiti wa wapiganaji hao kwa wiki kadhaa.
Mashambulizi hayo yalifanyika Jumamosi siku moja tu baada ya jeshi la Nigeria kutangaza makubaliano ya kusitisha vita kuwa yamefikiwa kati ya serikali na Boko Haram.
Kama sehemu ya makubaliano hayo, serikali ilisema wasichana 219 waliotekwa kutoka Chibok mwezi Aprili, wataachiliwa hivi karibuni.
Tangu tangazo hilo kutolewa, kundi hilo limeendelea kufanya mashambulizi, na hapajakuwa na kauli yoyote ikiwa wasichana wa Chibok wameachiliwa.
Kulingana na serikali, mazungumzo yalitarajiwa kufanyika kati ya serikali na Boko Haram, wiki hii nchini Chad.
Wakati huo huo, polisi wanasema kuwa shambulizi lililofanywa katika jimbo la Bauchi liliwaua watu watano.
Mashambulizi yoyote yanayofanywa kaskazini mwa Nigeria hulaumiwa kundi la Boko Haram. Hata hivyo kundi hilo kwa kawaida halijibu haraka na kwa hivyo huwa vigumu kuthibitisha ukweli kama ni wapiganaji hao waliofanya mashambulizi hayo au la.
0 comments:
Post a Comment