Friday, October 24, 2014

Friday, October 24, 2014
uda
CHAMA cha Kutetea Abiria (Chakua), kimeitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuyakamata magari ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), kutokana na kampuni hiyo kutokuwa na leseni ya kuendesha biashara ya usafirishaji.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chakua, Hassan Mchanjama, alisema hajui sababu ambazo zimeifanya Sumatra hadi leo kushindwa kuchukua hatua za kisheria za kuyakamata magari ya kampuni hiyo wakati inaujua ukweli.
Alisema wameitaka Sumatra kufanya hivyo, kwa sababu chama hicho kimejiridhisha kuwa UDA haina leseni baada ya kufanya uchunguzi na kubaini inafanya biashara hiyo ya usafirishaji kwa kutumia kibali kilichotolewa miaka 30 iliyopita.
“Kibali wanachotumia ni cha miaka mingi ambacho kimetolewa tangu enzi za aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela, wakati huo Sumatra haijazaliwa, hii ni ajabu na hata Sumatra ilipoanzishwa mwaka 2006 imeshindwa kuhoji,” alisema Mchanjama.
Mchanjama, alisema kwa sheria na utaratibu wa sasa kila anayetaka kufanya biashara ya usafirishaji abiria anapaswa kuomba leseni Sumatra jambo ambalo UDA haijafanya.
“Hizi taarifa tumezifanyia uchunguzi na wala hazina wasiwasi wowote, tutashangaa kama Sumatra itasema UDA inayo leseni ya kufanya biashara hii katika kipindi hiki,”alisema.
Aidha alisema UDA imekuwa ikikaidi kutekeleza sheria za Sumatra na kutolea mfano kuwa hadi leo haitaki kupiga mkanda kama daladala nyingine, kuandika nauli ubavuni na kibaya zaidi imekuwa ikitoza nauli inayotaka huku ikijiamulia kwenda njia inayotaka.
Mchanjama, alisema kampuni hiyo imefanya hivyo kwa miaka mingi kitendo ambacho ni makosa, akibainisha kuwa nyuma ya Sumatra na UDA kuna mambo mengi.
Alipotafutwa Ofisa Mfawidhi Sumatra wa Kanda ya Mashariki Dar es Salaam, Conrad Shio, ili kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo, alikiri kuwa kwa miaka nane tangu ilipoanzishwa Sumatra, kampuni ya UDA ilikuwa haijaomba leseni, bali ilikuwa ikitumia leseni maalumu iliyoipata awali.
“Hata hivyo, baada vikao vingi vilivyofanyika kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sumatra na UDA kuhusu mvutano huu imeamuliwa waendelee kutoa huduma huku ikitakiwa kuendeleza mchakato wa kuomba leseni kwa magari yake yote,” alisema Shio.
Hata hivyo, Shio alisema UDA imekamilisha hatua za maombi ya leseni ya magari 115 ambayo yameanza kupewa leseni.
Naye Meneja Uhusiano wa UDA, George Maziku, alisema; “Tunashukuru kama wametambua hivyo kuwa hatukuwa na leseni yao, lakini hatukuwa tukiendesha biashara hii bila kufuata sheria, bali tulikuwa tukifanya kazi kwa kutumia kibali ambacho tulipewa tangu mwaka 1974, utambue kuwa Sumatra haiifikii UDA,” alisema Maziku.
CHANZO: Tanzania Daima

0 comments: