Thursday, October 2, 2014

Thursday, October 02, 2014

Rais Jakaya Kikwete, akizindua barabara ya Tegeta - Mwenge jijini Dar es Salaam jana yenye urefu wa kilomita 12.9. Kushoto ni Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada na kulia ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee. 

Rais Jakaya Kikwete amesema tatizo la msongamano wa magari katikati ya jiji la Dar es Salaam haliwezi kuondoka, kutokana na uwezekano wa kupanua barabara zinazopakana na maghorofa kutokuwapo.
Alisema hayo alipohutubia sherehe za ufunguzi rasmi wa upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo sehemu ya Mwenge-Tegeta, yenye urefu wa kilomita 12.9, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema tatizo la msongamano wa magari haupo peke yake katikati ya jiji la Dar es Salaam, lipo katika miji yote mikubwa duniani, kama vile Washington (Marekani), Kuala Lumpur (Malaysia), Paris (Ufaransa), Roma (Italia), London (Uingereza) na Japan, na kwamba jawabu la kuiondoa halipo kutokana na barabara zake kupakana na maghorofa.

Alisema msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam unachangiwa na hatua ya maendeleo iliyopo hivi sasa nchini ikilinganishwa na miaka 20 iliyopita, ambayo imefikia katika baadhi ya familia kila mtu kumudu kumiliki gari.
“Na hakuna namna, tatizo hilo litaendelea kuwa kubwa zaidi mbele ya safari. Pale panapowezekana patarekebishwa, lakini kuna maeneo hayatawezekana. Lile eneo la katikati ya mji msongamano hautaondoka labda ubomoe maghorofa, upanue barabara tatu, haitawezekana,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema serikali imeona kuwa ufumbuzi, ambao unaweza kupunguza tatizo hilo ni kuongeza usafiri wa umma ili watu wasipate kishawishi cha kutumia magari yao binafsi na kwamba kwa Dar es Salaam, Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) unaoendelea kutekelezwa utasaidia suala hilo.
Alitaja njia nyingine za kupunguza tatizo hilo ni kuwapo usafiri wa treni, kutengeneza barabara za juu (flyover) kwenye maeneo ya makutano ya barabara, kama vile Tazara, Ubungo mataa na Kamata.
Njia nyingine ni kupanua barabara zinazonguka miji, kuanzisha usafiri wa baharini na kujenga miji mingine, kama vile Mabwepande, Kigamboni na Luguruni ili kuzuia watu kwenda maeneo ya katikati ya jiji kutafuta huduma. Aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuitunza miradi hiyo, kwani zimetumika gharama kubwa kuitekeleza.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, alisema mradi wa upanuzi wa barabara hiyo umegharimiwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Jica Sh. bilioni 12.1 Serikali ya Tanzania imechangia Sh. bilioni 7.62.
Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, alisema serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania, ikiwamo kusaidia kupunguza tatizo la msongamano wa magari barabarani.

CHANZO: NIPASHE
    

0 comments: