Dira ni kuwa na katiba bora itakayojenga Tanzania yenye demokrasia
ya kweli, uhuru wa kweli na maendeleo endelevu kwa watu wake wote.
Lakini uharamia katika mchakato wa katiba mpya umelipasua taifa. Mpasuko
huu unaweza kuwa mgogoro hasi wenye madhara kwa wananchi au mgogoro
chanya utakaoleta mabadiliko nchini.
Maharamia wanashangilia kilevi katika Bunge Maalum baada ya
kukamilisha uharamia dhidi ya rasimu ya katiba ya wananchi kwa kupata
theluthi mbili kwa njia za kiharamia. Katiba iliyopendekezwa kiharamia
na kudharau maoni ya wananchi ni katiba haramu iliyokosa maridhiano na
muafaka wa kitaifa.
Katiba haramu, katiba ya maharamia, katiba ya mafisadi, katiba ya CCM
wahafidhiana na mawakala wake inapaswa kupingwa mtaani na mahakamani
kwa mbinu mbalimbali.
Iwe ni kwa mikutano, migomo, maandamano, mashtaka au katika sanduku
la kura. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba mchakato huu wa mabadiliko ya
katiba ni mwanya wa mabadiliko katika taifa letu.
Theluthi mbili ilianza kutafutwa tangu wakati wa kutungwa kwa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, tulipinga muundo wa Bunge Maalum na uteuzi
wake; madhara yake yamedhihirika sasa.
Rais Kikwete akaongezea udhaifu huo kwa kutumia madaraka vibaya
kuteua wanaCCM mahafidhina na mawakala wao kwa wingi katika uteuzi wa
wajumbe wa kundi la 201 kuongezea katika hodhi haramu ya wabunge na
wawakilishi wa chama chake.
Sitta akakamilisha uharamia huo kwa marekebisho haramu ya kanuni za
Bunge Maalum ambayo yaliruhusu kura kupigwa nje ya Bunge hilo na mianya
mingine ya wizi wa kura.
Jana Oktoba Mosi Sitta alilalamikia hatua yangu ya kumtaja yeye,
Chenge na wenzake kuwa ni ‘maharamia’ dhidi ya rasimu iliyotokana na
maoni ya wananchi. Kwa kuwaita maharamia Sitta amelieleza Bunge Maalum
kuwa ni “siasa za kichuo chuo” na kwamba “hatuwezi kushika madaraka kwa
mbinu za kitoto”.
Nimkumbushe Sitta na maharamia wenzake kwamba mwaka 1958 Mwalimu
Julius Nyerere alishtakiwa kwa kuwaita ‘mashetani na maharamia’ wakuu wa
wilaya wa Serikali ya mkoloni. Ninapolitazama Bunge Maalum nakumbuka
utetezi wake mahakamani wa kukiri kutamka maneno hayo kwa lengo la
kuitaka serikali ya kikoloni itupie macho malalamiko ya watu.
Sitta na maharamia wenzake kama wameshindwa hata kuelewa waraka wa
viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi”,
ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa.
Leo Sitta, Samia Suluhu na maharamia wengine wanasherehekea kama
walevi ushindi wa muda mfupi walioupata kwa njia za kiharamia ikiwemo
kwa kuwashinikiza na kuwarubuni baadhi ya wajumbe kuhalalisha rasimu
haramu. Andrew Chenge aliyetajwa kwenye orodha ya mafisadi (list of
shame) ndiye aliyeongoza kazi hiyo kuanzia katika Kamati ya Uandishi.
Uharamia huu dhidi ya rasimu ya tume ya mabadiliko ya katiba na maoni
ya wananchi unapaswa kuwa kiunganishi kwa umma kutambua kwamba umoja wa
ukweli na uadilifu unapaswa kuvuka mipaka ya vyama, dini, pande mbili
za Muungano na tofauti zingine.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umeonyesha msimamo wake,
Mwenyekiti na Wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
wameonyesha msimamo wao, baadhi ya viongozi wa dini wameonyesha msimamo
wao, baadhi ya wanaharakati wameonyesha msimamo wao, baadhi ya wajumbe
ndani ya Bunge Maalum wameonyesha msimamo wao; wewe je?
Namna pekee ya kuirejesha rasimu ya katiba ya wananchi katika hali
iliyofikia ni kuikataa katiba haramu na kuwakataa wote waliofanya
uharamia kuwezesha rasimu hiyo kupendekezwa na wote watakao itetea
katiba hiyo.
Muasisi wa CCM alikiambia chama hicho mwaka 1995 kwamba “watanzania
wanataka mabadiliko wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM”.
CCM imepoteza mwanya wa kuwapa watanzania mabadiliko kutoka ndani ya
chama hicho.
Uharamia uliofanywa katika Bunge Maalum una baraka za Katibu Mkuu wa
CCM Kinana na Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete. Uharamia huo ulilenga
kuwezesha Maoni ya CCM yaliyopitishwa na vikao vya juu vya CCM kinyume
na maoni ya wananchi. Hatimaye kwa njia za kiharamia wajumbe wanaojiita
walio wengi wa CCM wamepitisha katiba haramu iliyopendekezwa.
Mwalimu Nyerere aliandika katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya
Tanzania kwamba Rais wa wakati huo Mwinyi alikuwa mtu mwema na mpole
lakini “kiongozi dhaifu”. Akamtakia heri na kuomba asaidiwe amalize
kipindi chake salama. Akatabiri kwamba chini ya CCM na uongozi wake
mbele ni giza tororo.
Rais Kikwete alithubutu kwa kukubali mchakato wa mabadiliko ya katiba
kuanza lakini ameshindwa. Na kwa udhaifu alio uonyesha, kwa vyovyote
vile mchakato huu hauwezi kusonga mbele na kukamilika chini yake.
Udhaifu pekee anao weza kuupunguza kwa sasa ni kusimamia marekebisho
ya 15 ya Katiba ya mwaka 1977 kuwezesha uchaguzi huru na haki katika
uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais mwaka 2015 na kuendelea kwa
mchakato wa katiba mpya mwaka 2016 kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Tumtakie heri Rais Kikwete amalize kipindi chake salama; matokeo ya
kura ya katiba haramu iliyopendezwa yatafutwa kwa kupingwa mahakamani
ama kwa njia nyingine.
Mahakama kwa kukosa uhuru wa kikatiba isipotimiza wajibu huo wa
kusimamia haki kwa wakati; katiba haramu iliyopendekezwa itafutwa kwa
sheria maalum itayotungwa na Bunge litakaloongoza nchi baada ya uchaguzi
2015.
Ikiwa watawala wa sasa au wa wakati huo watalazimisha katiba haramu
kwenda kupigiwa kura ya maoni, ni wazi itapigiwa kura ya hapana na
wananchi iwe ni mwaka 2015 au 2016.
Mabadiliko yatafutwe kwa kuwakataa watetezi wote wa katiba haramu
kuanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji mwaka
2014. Mabadiliko yatafutwe kwa kutaka Tume itangaze ratiba ya
uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2014 ili kila
mwenye umri wa kupiga kura ashiriki kufanya mabadiliko kupitia uchaguzi
2015 na kura ya maoni.
Kwa wajumbe mlioshiriki kuandika katiba haramu, naheshimu na
nakubaliana na maneno ya Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba kwamba tutakutana mtaani.
Dhima ni kuwa na katiba mpya itayoleta uongozi bora, sera sahihi,
mikakati makini na Muungano na Muundo wa Utawala thabiti kwa maendeleo
endelevu.
Nyinyi mkiwa na katiba haramu sisi tutakuwa na rasimu ya wananchi;
sauti ya watu, ni sauti ya Mungu hivyo umma utaamua na historia itatoa
hukumu kwa maharamia na walevi wa madaraka.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi.
John Mnyika (Mb)
02/10/2014
Chanzo: Jamii Forums.
0 comments:
Post a Comment