KITUO cha Polisi Kimara Mwisho Jumamosi kilifungwa baada ya askari wa kituo hicho kuwekwa mahabusu kwa madai ya kuuza kidhibiti cha mirungi waliyoikamata.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kilichoomba kuhifadhiwa jina kwa usalama wake, askari wa kituo hicho waliwekwa mahabusu mwishoni mwa wiki katika Kituo cha Mbezi Luis jijini Dar es Salaam, baada yakwenda kinyume na maadili ya kazi na kusababisha kifungwe Jumamosi na kufunguliwa jana majira ya saa tatu asubuhi.
Chanzo hicho, kilisema askari hao walimkamata mtuhumiwa aliyekuwa na mzigo wa mirungi, ambaye inadaiwa walimlazimisha awape sh 200,000 ambazo alikubali.
Hata hivyo, waliendelea kudai kiasi nyingine kwa madai kuwa sh 200,000 alizotoa awali zilikuwa ni kwa ajili ya OCD, na kwamba na wao wanataka za kwao ili mambo yaishe.
Mmiliki wa mirungi hiyo, aliwaomba wampe nafasi ili aende nyumbani akachukuwe fedha kwa sababu kipindi hicho hakuwa nazo, ambako walimruhusu.
Aliporudi hakuwakuta, hivyo kuamua kuwapigia simu, lakini wakawa wanamsumbua kwa kila maeneo waliyokuwa wakimueleza wako alipofika hakuwakuta.
Baada ya kuona usumbufu huo, aliamua kwenda kituo cha Mbezi kutoa taarifa, na askari hao kuitwa na walipoulizwa mzigo walioukamata uliko, walikiri mbele ya OCD kuwa wameuza, kitendo kilichosababisha watiwe rumande.
Mmoja wa polisi wa kituo hicho cha Mbezi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa madai kuwa si msemaji, alisema hayo ni majungu kwani hakuna tukio hilo.
“Huyo muongo, mmemhoji vizuri…hata kama kilifungwa kitakuwa kimefungwa kwa sababu nyingine na hatuwezi kumueleza kila mtu.
“Wakihitaji kujua kimefungwa kwa sababu gani waje huku tutawaambia, watu kama hao muwe na tahadhari nao, namba zetu zipo kwanini wasitupigie baadala yake wanakuja huko, ina maana wamekuja kutuchomea,” alisema polisi huyo.
Aliongeza kuwa kituo cha Kimara kinafanya kazi saa 12 na sio 24 kama walivyozoea wananchi, ingawa baadhi ya siku kinatoa huduma saa 24 kwa sababu panalazwa mahabusu.
Alipotafutwa Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita muda mrefu bila ya kupokelewa.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment