Friday, October 31, 2014

Friday, October 31, 2014

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji.Kigali. Kwa siku zaidi ya 10 sasa, Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limeshindwa kuendelea na vikao vyake mjini hapa kutokana na wabunge wake kugomea vikao hivyo vya mkutano wa pili, wakishinikiza kuchukukuliwa hatua kwanza kwa mmoja wa wabunge wake, Shy-Rose Bhanji wa Tanzania.Bunge hilo lilianza vikao vyake Oktoba 20, mwaka huu likitarajiwa kujadili na kupitisha miswada kadhaa ya sheria pamoja na taarifa za kamati, lakini hadi jana hakuna kazi hata moja kati ya hizo iliyokuwa imefanyika kwa ukamilifu, kutokana na mgomo unaoendelea huku likitarajiwa kuhitimisha kazi zake leo.Miongoni mwa kazi zilizokuwa zimepangwa kufanyika ni pamoja na kujadili na kupitisha muswada wa Sheria ya Ushirika wa Afrika Mashariki na kupokea taarifa za Kamati ya Masuala ya Jumuiya na Utatuzi wa Migogoro, Kamati ya Sheria, Kanuni na Haki, Ripoti ya Kamati ya Hesabu zilizokaguliwa za EAC kwa mwaka wa 2012/13 pamoja na taarifa iliyoitwa nyeti ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (CTI).Vikao vyote ambavyo vimefanyika kwa ajili ya kuliwezesha Bunge hilo kutekeleza kazi hizo, vimekuwa vikiahirishwa baada ya dakika kati ya 20 na 30 kutokana na baadhi ya wabunge kutumia kanuni ya 31 kutoa hoja ya kutaka mjadala kuhusu Bhanji ufanyike kwanza kabla ya kuendelea na shughuli nyingine.Mjumbe wa Tanzania ambaye ni mwenyekiti wa CTI, Angela Kizigha alisema taarifa ya kamati yake haikujadiliwa baada ya wabunge kutaka kwanza suala la nidhamu lipewe nafasi. “Hiyo ndiyo hali halisi, walikataa na mimi sikuwa na jinsi ya kulazimisha,” alisema.Gazeti hili limebaini kuwa baadhi ya wabunge wanaoshinikiza kujadiliwa kwa suala la Bhanji, wanataka kwanza aondolewe katika ujumbe wa Kamishna wa Bunge hilo na baadaye asimamishwe kushiriki katika vikao vya Eala kwa kadiri muda utakavyoamuliwa.Juzi alasiri, Spika wa Bunge hilo, Dk Margaret Zziwa alitoa taarifa kwamba Oktoba 21 na 22, 2014 Tume ya Eala ilikutana na kujadili suala la utovu wa nidhamu wa baadhi ya wabunge wake, lakini ilishindwa kulihitimisha kutokana na ukubwa wa tuhuma husika huku akiahidi kuwa suala hilo lingejadiliwa tena jana.“Kwa kuwa mambo yaliyohusishwa ni mazito, hayakuweza kupata hitimisho, suala hili litajadiliwa tena kesho (jana), Jumatano Oktoba 29, 2014 wakati wa kikao cha tume na hatua zitakazochukuliwa mtajulishwa,” alisema Dk Zziwa.Tuhuma zakeBhanji anatuhumiwa kwamba aliliaibisha Bunge hilo wakati wa ziara ya nchini Ubelgiji iliyowashirikisha wajumbe wa tume na wenyeviti wa Kamati za Bunge hilo na kwamba alifanya fujo ndani ya ndege kwa kutoa lugha chafu kwa wabunge wenzake pamoja na kutoa matamshi yasiyo ya staha katika hafla iliyoandaliwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Dk Diodorus Kamala.Juzi baada ya kikao cha Eala kuahirishwa dakika 30 tangu kilipoanza, wabunge wa Tanzania walikutana kwa zaidi ya saa mbili katika moja ya kumbi za Bunge la Rwanda, kujadili hatima ya mwenzao, kikao ambacho hata hivyo hakikuwa na mwafaka wa pamoja.Mmoja wa wabunge hao, Makongoro Nyerere alisema wameshindwa kuwa na mjadala wa kina na baadaye kutoa msimamo kuhusu suala hilo kwa sababu Bhanji hakuwa amepewa tuhuma rasmi zinazomkabili, badala yake kumekuwa na malalamiko ya mdomo tu.CHANZO: Mwananchi


0 comments: