BUNGE limepeleka kamati ndogo, chini ya uongozi wa Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, kwenda kuchunguza mauaji ya kutisha yanayoendelea kutokea wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Hatua hiyo ilitangazwa jana Bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akitoa taarifa ya Serikali kuhusu hali tete ya mauaji wilayani Kiteto.
Alisema taarifa ya Kamati ya Ole Sendeka, itawasilishwa ili jambo hilo sasa lijadiliwe na Bunge.
“Na imani yangu ni kwamba, taarifa ile itawasilishwa baadaye kwa ajili ya kujadiliwa hapa bungeni. Lakini kutokana na matukio ambayo yanaendelea pale Kiteto, bunge kupitia Kamati ya uongozi, liliona ni vizuri serikali iseme kinachoendelea ni nini, ili tuweze wote kupata picha kamili,” alisema Pinda.
Akizungumzia hali ilivyo Kiteto, Pinda alisema matukio ya mauaji hayo yameanza hata kuhusisha matumizi ya silaha za kisasa kutoka zile za jadi.
Migogoro hiyo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku hasa nyakati za kiangazi, ambako malisho hupungua na kuenea katika takribani kwenye Wilaya zote zenye wakulima nchini.
Alisema kuongezeka kwa migogoro pamoja na mambo mengine, kunatokana na kuongezaka kwa idadi ya watu na mifugo na kusababisha rasilimali ardhi, maji na miundombinu kutotosheleza mahitaji.
“Hali hiyo inaongezewa makali na mabadiliko ya tabia nchi na kulazimisha wafugaji na wakulima kuhamahama bila kuzingatia taratibu… Kwa ujumla, migogoro hii iko ndani ya jamii ya asili na inahusisha makundi mbalimbali ya jamii, ugomvi mkubwa ukiwa ni rasilimali hususan maji na malisho,” alisema.
Akizungumzia mauaji ya hivi karibuni, Pinda alisema Novemba 11 mwaka huu, majira ya saa 11 jioni katika kijiji cha Matui, yaliibuka mapigano kati ya wakulima na wafugaji ambayo yalisabaisha mauaji ya watu watano.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni kutokana na baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye shamba la mihogo ya mkulima, Mzee Hassan.
“Mzee huyo katika kufuatilia haki yake, kutokana na kuharibiwa shamba lake, alitekwa na kuuawa na mwili wake kuonekana alfajiri ya tarehe 12 Novemba.
“Baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa mzee huyo, ndipo mauaji ya kulipizana kisasi baina ya wakulima na wafugaji yalipofanyika. Pamoja na uharibifu wa mali. wananchi watano waliuawa katika tukio hilo, Mzee Hassa (65), mkulima na Mrangi, Maria (35) Mmasai, Job Nsagu (48) Mgogo, Julius Andrea (52) Mrangi na Mmasai mmoja ambaye mpaka wakati taarifa hiyo inatolewa ilikuwa haijafahamika,” alisema.
Kwa mujibu wa Pinda, Januari 12 mwaka huu, yalitokea mauaji ya wananchi 10 wilayani Kiteto, baada ya mapigano kati ya wafugaji na wakulima waliokuwa wakigombea kumiliki eneo la hifadhi ya jamii ya Embolei Murtangos.
Alisema wakati juhudi za kurejesha amani katika eneo la Matui zikiendelea, vurugu nyingine zilijitokeza Novemba 13 katika kijiji cha Chekanao ambapo wazee wawili waliuawa na maboma ya kimasai 13 yalichomwa moto.
“Serikali haipendezwi na hali hiyo na itafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanaohusika wote wanakamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria,” alisema.
Pinda, alisema idadi ya polisi imeongezwa katika wilaya hiyo ili kukabiliana na aina zozote za uvunjifu wa amani, hakuna taarifa zingine za vifo, zilizotokea kati eneo la hifadhi ya Murtangos, tangu alipofanya ziara wilayani kiteto.
0 comments:
Post a Comment