MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, amepata Tuzo ya Mafanikio ya Kutukuka Maishani (AABLA).
Tuzo hiyo alikabidhiwa mwishoni mwa wiki katika fainali za CNBC All Africa Business Leadership Awards (AABLA), jijini Johannesburg Afrika Kusini, mbele ya wafanyabiashara maarufu kutoka Afrika na maeneo mengine duniani.
Tuzo ya Mafanikio ya Kutukuka Maishani, hutolewa kwa mtu ambaye amefanya vyema katika kutekeleza maono ya kibiashara katika bara la Afrika na kuonyesha uthubutu na ujasiri katika kuwezesha mafanikio.
Katika hotuba yake ya kukubali tuzo hiyo, Dk. Mengi alisema anaitoa tuzo hiyo kwa vijana wa Afrika kwa lengo la kuwataka wajiamini kwamba, wao pia wanaweza kuleta mabadiliko kwa kutupilia mbali minyororo ya umaskini.
Aliwaambia vijana hao wajasirimali kwamba, wanachohitaji wao ni utambuzi wa kuona fursa zilizopo na kuwa tayari kufanyakazi kwa bidii na kutokata tamaa.
Tuzo ya mfanyabiashara wa mwaka ilitwaliwa na Ofisa Mtendaji wa EOH ya Afrika Kusini, Asher Bohbot, wakati tuzo ya mfanyabiashara mwanamke imekwenda kwa Ofisa Mtendaji wa Keroche Breweries ya Kenya, Tabitha Karanja.
Gil Oved na Ran Neu-Ner ambao ni maofisa watendaji wa kampuni ya ushauri wa masoko ya Afrika Kusini, Creative Counsel, walinyakua tuzo ya wafanyabiashara vijana wakati mwanzilishi wa kampuni ya uwekezaji, Brimstone Investment Corporation, Fred Robertson alipata Tuzo ya Mjasiriamali wa mwaka.
0 comments:
Post a Comment