Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP
Ernest Mangu akimsikiliza Diwani wa Kata ya Matui Wilayani Kiteto
Bw.Athuman Kidawa wakati alipofanya ziara Wilayani humo kufuatia kuwepo
kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji uliopelekea
kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa vifo.Kushoto ni Afisa
tarafa wa Matui Bw.Eliakimu Ndelekwa.(Picha na Frank Geofray wa Jeshi la
Polisi)
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP
Ernest Mangu akizungumza na wananchi wa Kata ya Matui Wilayani Kiteto
wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya
ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano
yaliyosababisha kutokea kwa vifo. (Picha na Frank Geofray wa Jeshi la
Polisi)
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP
Ernest Mangu akizungumza na Mtendaji wa Kijiji cha Chekanao, Kata ya
Kiperesa , Wilayani Kiteto Bw.Omar Ndee (kulia) wakati alipofanya ziara
wilayani.Katikati ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Deusdedit
Nsimike pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw.Japhet Chafu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini
IGP Ernest Mangu ameahidi kuongeza idadi ya Askari katika kijiji cha
Chekanao, kata ya Kiperesa wilayani Kiteto Mkoani Manyara kufuatia
wananchi katika kijiji hicho kujitolea nyumba kwa ajili ya kuishi Askari
kwa lengo la kuimarisha usalama katika maeneo yao kufuatia kuwepo kwa
migogoro ya ardhi inayosababisha kutokea kwa mauaji.
IGP Mangu aliyasema hayo jana
wakati alipokuwa katika ziara Wilayani Kiteto ya kujionea uharibifu
uliojitokeza pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo iliyopelekea
kutokea kwa vifo vya wakulima na wafugaji hivi karibuni katika wilaya
hiyo ambapo watu kadhaa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na
vurugu hizo.
Alisema kufuatia kuwepo kwa
umbali mrefu wa kituo cha Polisi na kijiji hicho atahakikisha askari wa
kudumu wanakuwepo ili kushirikiana na wananchi katika kuwabaini wahalifu
wanaofanya vurugu na kuendeleza migogoro hiyo ambapo wananchi nao
waliahidi kujenga kituo cha Polisi.
Kwa upande wake Mtendaji wa
Kijiji cha Chekanao Bw.Omar Ndee alisema wamekuwa wakipata shida
kutokana na umbali mrefu wa kituo cha Polisi jambo ambalo limekuwa
likifanya kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu vinavyochangiwa na migogoro
ya ardhi katika wilaya ya Kiteto.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho
Japhet Chafu alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuimarisha usalama
kijijini hapo tangu kutokea kwa mauji ya wakulima na wafungaji ambapo
alibainisha kuwa bila kuwepo wao hali ingekuwa mbaya zaidi kutokana na
kutokuwepo na muafaka baina ya wakulima na wafugaji.
“IGP hawa askari wako
wasingekuwepo hapa usingekuta mtu lakini tunawashukuru sana hawa askari
kwa kuwa hivi sasa hali ya usalama imerejea na hata shambani tumeanza
kwenda” Alisema Bw.Chafu.
IGP Ernest Mangu alitumia ziara
hiyo kuzungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, kamati ya ulinzi na usalama
ya wilaya, Wakaguzi wa Tarafa pamoja na Askari Kata ili kutafuta
ufumbuzi wa migogoro hiyo na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama.
0 comments:
Post a Comment