Mh. Zitto Kabwe Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
Ripoti hiyo iliyotokana na uchunguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), tayari imetua mikononi mwa Spika wa Bunge na jana ilikabidhiwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA).
Zitto ambaye aliwasili jana mjini hapa na kuingia moja kwa moja kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi, alisema baada ya kikao hicho atajua Kamati yake itakutana lini na uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili waweze kufanya kazi yao vizuri.
Mbunge huyo (Zitto) naye anadaiwa kugawiwa fedha za IPTL sh milioni sita kwa ajili ya matibabu ya marehemu mama yake Shida Salum, aliyetakiwa kupelekwa nchini India
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Zitto alisema watu wanaowashambulia katika kusimamia sakata la upotevu wa fedha za Tegeta Escrow wamepewa pipi kwa nia ya kuwaondoa watanzania katika mstari, huku waliowapa pipi hizo wakiwa wanafaidi mabilioni ya watanzania.
Alisema kutokana na suala hilo kuwa tishio kwa viongozi mbali mbali, baadhi yao wamekubali kupewa pipi (jojo) na kujitahidi kuwaaminisha Watanzania kuwa wanaofuatilia kadhia hiyo hawana nia njema.
“Jambo la ajabu kuwaona wanasiasa wanaokubali kuuza utu wao kwa pipi pasipo kujua ukweli wa mustakabali wa fedha za Tegeta Escrow utakuwa na manufaa makubwa kwa watanzania wote” alisema
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa ripoti ya CAG, imebaini kuwapo makosa yaliyofanywa na Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Uchumi pamoja na BoT katika kuruhusu uchotwaji wa fedha hizo kinyume cha taratibu.
Habari zaidi zinasema kuwa ripoti hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu na wabunge wote bila kujali itikadi zao, imewataja baadhi ya watendaji wa wizara na taasisi hizo kwamba ndio waliohusika katika kashfa hiyo inayolitikisa taifa kwa sasa.
Ripoti hiyo ambayo imepangiwa kujadiliwa Bungeni Novemba 26 na 27 mwaka huu, haijamtaja Waziri Mkuu Mizengo Pinda wala ofisi yake kuhusika na kashfa hiyo.
Licha ya Pinda kutotajwa kwenye ripori hiyo ndani ya Bunge kuna shinikizo kubwa la wabunge la kumtaka awajibike kwa madai ya kushindwa kuzuia watendaji walio chini yake kuruhusu uchotwaji wa mabilioni hayo ya fedha.
Hoja hiyo inashabihishwa na kilichompata mtangulizi wake, Edward Lowasa aliyejiuzulu mwaka 2008, kwa kashfa ya Richmond.
Ripoti yazidisha hofu kwa vigogo
Kuwasili kwa ripoti hiyo bungeni kumezidisha hofu kubwa kwa vigogo watuhumiwa wa kashfa hiyo, huku wadadisi wa mambo ya siasa wakianikiza kwamba kuna hatari ya serikali kuanguka.
Watuhimiwa katika kashfa hiyo iliyosababisha wahisani kusitisha misaada yake nchini ya zaidi ya sh trilioni moja ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospiter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi ambao imeelezwa kuwa wanafanya kila aina ya ushawishi kuhakikisha wanaepuka kikombe hicho.
Wengine ni Gavana wa Benki Kuu (BoT) Benno Ndullu, Waziri wa Fedha na Uchumi Saada Mkuya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Frederick Werema na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Felchesmi Mramba huku Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijatwa kuhusika kutokana na uzembe wa watendaji wake.
Ndani ya Bunge wiki hii, kashfa ya Escrow akaunti iliyotokana na mradi wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd, (IPTL) iliibuliwa mara tano kwa nyakati tofauti na wabunge tofauti ambao ujumbe wao ulikuwa kuishinikiza serikali ilete ripoti hiyo haraka Bungeni.
Kila kona ya eneo la viunga vya Bunge, mjadala na habari ya mji wa Dodoma ni kuhusu kashfa hiyo na hatma yake, huku baadhi ya wabunge wakihusisha kutokuwepo kwa wiki nzima bila taarifa kwa Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwamba huenda kunatokana na kashfa hiyo.
Hata hivyo habari kutoka ndani ya bunge zilisema kwamba, Waziri Mkuu Pinda alikuwa na majukumu mengine ya kikazi nje ya Bunge lakini kuhusu Werema, hakuwa na taarifa za kutokuwepo kwake ingawa jana alionekana kwenye viwanja vya Bunge.
Kutokuwepo kwa Jaji Werema bungeni kwa wiki nzima wakati joto la kashfa hiyo liko juu, kumemfanya Mbunge wa Kigoma Kusini aliyeishikia bango kashfa hiyo kutamba kwamba Tumbili kamfukuza mwizi Bungeni, akimaanisha yeye Kafulila aliyewahi kuitwa Tumbili na Jaji Werema, yeye (Kafulila) amemfukuza aliyemwita mwizi bungeni.
“Jaji Werema aliwahi kuniita mimi Tumbili ndani ya Bunge nami nilimwita Werema mwizi wa kashfa ya Escrow… sasa Tumbili amemfukuza Jaji Werema bungeni, maana hakai,” alitamba Kafulila.
Akizungumzia ripoti ya CAG iliyotua Bungeni, Kafulila, alisema ripoti hiyo itathibitisha ukweli wa kashfa hiyo kwani anajua kila kitu namna fedha hizo zilizovyochotwa.
Mgogoro uliosababisha fedha kuwekwa katika akaunti hiyo ya Tegeta ya BoT ulitokana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kugoma kulipa gharama za uwekaji mitambo (Capacity Charge) kwa IPTL mwaka 2006 kwa vile ilibainika IPTL ilikuwa ikitoza gharama kubwa kuliko iliyopaswa.
Akaunti hiyo ya Tegeta ilianzishwa kwa sababu ya kuhifadhi fedha zote zilizopaswa kulipwa na Tanesco hadi hapo mgogoro baina ya pande hizo mbili umalizike.
Hata hivyo, Septemba mwaka jana, serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, iliagiza BoT kulipa fedha hizo kwa kampuni ya PAP mara baada ya kuridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu uliosema kwamba mgogoro baina ya wamiliki wa IPTL na Tanesco umemalizika na hivyo Benki Kuu haina sababu ya kuhifadhi fedha hizo.
Uamuzi huo wa kulipwa ulizua upinzani mkali bungeni ambapo wabunge wawili wa kambi ya upinzani; Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, walidai kuwa zoezi hilo limejaa ufisadi na Bunge liliazimia kwamba suala la kutolewa fedha katika akaunti ya Tegeta lifanyiwe uchunguzi wa kina na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
CHANZO : Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment