Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk.Edward Hosea
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema imemhoji na inaendelea kumchunguza mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema vigogo wote waliohusika na sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanachunguzwa akiwamo Rugemalira.
“Tunawachunguza wote, hatuwezi kufanya kazi harakaharaka kama zimamoto, tunakwenda hatua kwa hatua, uchunguzi ukikamilika wote watakaopatikana na hatia watapelekwa mahakamani,” alisema Dk Hoseah.
Rugemalira akiwa mbia wa IPTL chini ya Kampuni ya VIP Engineering and Management (VIPEM), ndiye kiini cha vigogo wengi wa Serikali kupewa mgawo wa fedha kupitia Benki ya Mkombozi.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani alisema Rugemalira anachunguzwa na kueleza kuwa taratibu zote za uchunguzi ikiwamo mahojiano zimeshaanza kufanyika... “Tumeshamuhoji na tunaendelea kumchunguza, hilo linaeleweka.”
Walioburuzwa kortini na Takukuru
Mpaka sasa Takukuru imeshapeleka watuhumiwa kadhaa mahakamani wakiwamo maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Miongoni mwao ni Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa, Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Roman Urassa na Mkurugenzi wa Fedha BoT, Julius Rutta Angello ambao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya mamilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea anayedaiwa kupokea Sh161,700,00. Mwingine ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma ambaye anadaiwa kuwekewa kiasi cha Sh323 milioni.
Waliosombwa na escrow bungeni
Viongozi wengine Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja aliyekuwa akiongoza Kamati ya Sheria na Utawala na Mbunge wa Chunya (CCM), Victor Mwambalaswa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini walijiuzulu nafasi zao hizo kutokana na kashfa hiyo.
Chanzo: MWANANCHI
Chanzo: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment