Friday, March 20, 2015

Friday, March 20, 2015
                                  
Rais mstaafu wa awamu ya tatu,Benjamini Mkapa amezishauri nchi za Afrika na Tanzania ikiwemo,kuwa na mipango madhubuti inayotekelezeka katika mazingira ya kiafrika ya namna ya kutumia rasilimali zilizopo na kuongeza ubunifu kwa kutumia sayansi na teknolojia. 

Ameongeza kuwa hatua hiyo itaziwezesha nchi nchi za Afrika kujitegemea kiuchumi badala ya kutegemea misaada na mikopo kutoka taasisi za kimataifa kama benki ya dunia na shirika la fedha duniani IMF kwa kuwa hazikuundwa kwa ajili ya kuzisaidia nchi za kiafrika.


Ni siku ya pili ya uzinduzi wa kavazi la Mwalimu uliombatana na mijadala kabambe kuhusu namna ya kuliendeleza taifa kiuchumi kwa kutumia fikra za Mwalimu Nyerere,kwa kutumia ubunifu, sayansi na teknolojia ambapo rais huyo wa awamu ya tatu Benjamini William Mkapa,ambaye ni mmoja wa washiriki amesema nchi za kiafrika hazina mipango ya kujikwamua kiuchumi kutokana na changamoto kadha wa kadha tofauti na mataifa ya Ulaya yaliyokuwa na mipango ya namna ya kuziendeleza nchi zao baada ya vita vya kwanza na vya pili vya dunia ambapo Benki ya Dunia na Shirika la fedha la Duniani IMF ziliundwa kwa ajili ya kuyasaidia mataifa hayo.
Mkapa pia alisema kuwa, moja ya jambo ambalo linamnyima usingizi kwa kushindwa kulianzisha katika uongozi wake ili kusaidia idadi kubwa zaidi ya watanzania kuondokana na umasikini, ni uanzishwaji wa benki ya kilimo kutokana na idadi kubwa ya watanzania kutegemea kilimo ambacho kingewasaidia kuondokana na umasikini kwa kuwapa ruzuku na elimu ya kilimo cha kisasa.
Akizungumza kabla ya Mkapa, mmoja wa watoa mada amesema ni vizuri viongozi wa kiafrika wakaanza kufikiria namna ya kutatua matatizo ndani ya afrika hususani katika masuala ya usalama wa chakula, ajira kwa vijana kama yalivyokuwa mawazo ya mwalimu Nyerere wakati wa azimio la Arusha.
Mmoja wa wanazuoni walioshiriki katia kavazi la Mwalimu Prof Mwesiga Baregu amesema ukosefu wa uongozi adilifu unaotekeleza na kusimamia kile inachokisema ni changamoto kwa taifa kwa sasa na kwamba ni vyema kuangalia namna ya kupata uongozi adilifu unaojali mawazo na maoni ya wananchi tofauti na sasa ambapo tabaka tawala linataka kuwaamulia wananchi tofauti na matakwa yao.

0 comments: