Thursday, April 16, 2015

Thursday, April 16, 2015
 
Picha ikionyesha uteuzi wa wawakilishi mbali mbali wa Umoja wa Afrika 
uliofanywa hivi karibuni ambapo Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali (juu kulia) ambaye hivi karibuni ameteuliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dr. Nkosazana Dlamini Zuma kuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika nchini Sudani ya Kusini.


Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dr. Nkosanzana Dlamini Zuma, amemteua, Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ),kuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika Sudan ya Kusini .

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na AU na nakala yake kutumwa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, inaeleza kwamba makazi ya Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali yatakuwa Juba.

Pamoja na uteuzi wa Brigedia Jenerali Sara Rwambali, Dr. Nkosazana Dlamini Zuma pia amewateua Madame Josephine- Charlotte Mayuma Kala kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, anayekuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika huko Cote d’Ivoire na makazi yake yakiwa Abidjan.

Wengine walioteuliwa ni Madame Nyiramatama kutoka Rwanda, anayekuwa Mkuu wa Ofisi ya AU huko Chad , makazi yake yakiwa Ndjamena na Dr. Arvin Boolel kutoka Mauritius anayekuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya AU katika Maziwa Makuu Burundi na makazi yake yakiwa Bujumbura.

Taarifa kwa vyombo vya Habari kutoka AU inaeleza zaidi kwamba uteuzi huo ni sehemu ya AU ya kuhakikisha uwepo wake katika kila eneo na vile vile kuunga mkono juhudi zinazolenga katika kukuza Amani na Usalama Barani Afrika

“Ninatoa pongezi zake za dhati kwa wateuliwa ambao ni viongozi wa ngazi za juu na wenye sifa za kutukuka katika utumishi wa umma wakiwa na uzoefu mkubwa katika eneo la amani na usalama. Si jambo la ajabu kwamba wateule watatu kati ya wanne ni wanawake” anasema Dr. Zuma

Na kuongeza, “katika mwaka huu wa 2015, ambao Umoja wa Afrika umejikita katika uwezeshwaji wa wanawake. Ninayo matumaini makubwa kwamba AU na Afrika kwa ujumla itanufaika na utaalamu na uzoefu mkubwa na uwezo wa kiuongozi kutoka kwa wateuliwa hawa”.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU pia ametoa wito kwa wadau wote kuwapatia ushirikiano wateuliwa hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu kwa maslahi ya Bara la Afrika, huku akitoa shukrani kwa wawakilishi ambao wanamaliza muda wao.

0 comments: