Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa
ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa amesema Tanzania inahitaji Rais atakayefanana na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya misa ya maadhimisho ya Sikukuu ya Ijumaa Kuu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano jana jijini Dar es Salaam, Dk Mokiwa aliwataka Watanzania kutochanganywa na sura za watu wanaojitokeza kutaka urais.
“Katika kipindi hiki, najua sura nyingi zitajitokeza, nguvu za watu wenye fedha pia na kundi la vijana ndilo kubwa, lakini vijana hawapaswi kuchanganyikiwa, waungane na kupata kiongozi ambaye atatatua changamoto zao na ajenda yao kuu iwe ni ukosefu wa ajira,” alisema Askofu Mokiwa.
Alisema kundi kubwa la vijana linaweza kujengewa chuki kupitia vyama vyao, lakini akawataka kuungana katika kufanya uamuzi wa kiongozi ambaye atakuwa tayari kutatua changamoto zao, zinazosababisha wakate tamaa ya maisha na kujiingiza katika kutumia miili yao, kama makontena ya kubeba dawa za kulevya.
Alisema kiongozi wa aina ya Mwalimu Nyerere ndiye anayehitajika, ili akabiliane na changamoto mbalimbali zinazokabili wananchi, ikiwa ni pamoja na uchumi mbovu unaonufaisha nchi tajiri zaidi, upatikanaji wa maji, nishati na mfumo bora wa ukusanyaji kodi.
“Nchi inahitaji pia mfumo mzuri wa elimu utakaotufanya Watanzania tuwe na elimu bora tofauti na sasa msomi akiwa hapa anaonekana kasoma, lakini akitoka nje hawezi hata kuzungumza Kiinger eza akaeleweka,” alisema Askofu Mokiwa.
Alisisitiza Watanzania kuwa makini kupata viongozi watakaoboresha pia sekta ya afya na kuondokana na gharama za kusafirisha watu kwenda kupata matibabu nje ya nchi. “Tunataka India iwe hapa hapa nchini,” alisema.
Malasusa
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa alisema Wakristo wanapaswa kuishi maisha ya unyenyekevu na kusamehe, ili kuleta utofauti na watu wengine wasiomfahamu Mungu.
Akihubiri katika Ibada ya Ijumaa Kuu, Dk Malasusa alisema Wakristo wengi hawajui kusudi lao hapa duniani, ndio maana wanashindwa kuishi maisha ya unyenyekevu na msamaha kama Yesu Kristo.
Alisema tunda la unyenyekevu kwa wanadamu, limepungua wakati ni tunda la kiroho, ambalo mwanadamu anapaswa kuwa nalo tofauti na hali ilivyo sasa.
Viongozi
“Yesu alinyenyekea mbele za Mungu na sisi hapa tunamkiri Yesu, lakini unyenyekevu hakuna... wengine hapa wakishapewa nafasi fulani, basi unyenyekevu hakuna, hata kinafasi kidogo tu cha kuongoza anabadilika hapo hapo,” alisema.
Alisema ndio maana Wakristo wanashindwa kuishi kama Yesu na wala hawajui kusudi lao la kuwepo duniani na kutaka kila mmoja kujiuliza wapi wanajua nafsi zao zitakwenda, maana Yesu alijua ndio maana pale msalabani alimwambia Mungu mikononi mwako naiweka roho yangu.
Askofu Malasusa alisema kupitia Ijumaa Kuu, Yesu anafundisha tunda la msamaha, ambalo wanadamu wengi wanashindwa kwa kutosamehe waliowakosea.
“Pamoja na yote Bwana Yesu aliyotendewa alituombea kwa Mungu msamaha, jambo ambalo wengi wetu linatushinda... kusamehe ni tunda kutoka kwa Mungu mwenyewe,” alisema.
Alitoa mwito kwa Wakristo kujifunza kusamehe, ili kuleta utofauti na watu wengine na kwamba Mungu ametoa mwanawe wa pekee kufa kwa ajili ya wanadamu na kuwatoa kwenye uchafu kwani huyo ndio Mungu halisi wa msamaha.
Askofu Malasusa alisema Wakristo wakiwa watu wa msamaha, watavuta watu wengi kwa Yesu Kristo na kuwataka waumini wote kuomba katika Ijumaa Kuu ili iwe na faida katika maisha yao.
Macho ya watu
Naye Paroko wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Audax Kaasa alisema kuna viongozi nchini ambao wanafahamu kuwa baadhi ya mambo hayafai, lakini wanaogopa kusema ukweli kwa kuogopa macho ya watu.
Akihubiri katika Misa ya Ijumaa Kuu kanisani hapo, alitaka waumini wawaombee viongozi ili wawe na hofu na Mungu na kusimamia ukweli.
“Hata sasa kuna viongozi kama Pilato, ambaye alijua kuwa Yesu Kristo hakuwa na kosa, lakini alimhukumu kwa kuogopa macho ya watu, viongozi hao wapo na wanajua ukweli wa jambo fulani lakini wanaogopa macho ya watu,” alisema.
Alisema kwa sasa nchi inahitaji watumishi waadilifu ambao wanasimamia ukweli bila kujali macho ya watu, ili kuweka wazi mambo yote yanayohusu jamii.
Pia, aliwataka Watanzania kuwa na moyo wa kusamehe na kuvumilia, huku wakiomba msamaha kwa jambo lolote wanalokosea na siyo kukata tamaa.
Nia mbaya
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu, amewataka Watanzania kuzidi kuombea Taifa liwe na amani na wote wenye nia mbaya na nchi, Mungu awafichue na kuwaumbua waziwazi.
Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Redio Maria baada ya Misa ya Ijumaa Kuu iliyofanyika Katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu Tereza, Jimbo Kuu la Arusha.
Amesema neno lake kuu kwa Wakristo na Watanzania wote, ni kuweka misingi ya amani mioyoni mwao, ili waieneze amani hiyo kwa familia, jamii inayowazunguka na nchi nzima.
Askofu Lebulu alisema kuna watu wachache wenye nia mbaya katika jamii na kuongeza kuwa anamuomba Mungu, ili wafichuliwe popote walipo na kuwekwa wazi ili kuzuia matendo maovu yanayohatarisha amani ya nchi.
Aliwataka waumini wasichoke kuomba amani, kwa kuwa ni kwa sala pekee, Mungu atailinda nchi dhidi ya hila mbaya.
0 comments:
Post a Comment