Wednesday, July 22, 2015

Wednesday, July 22, 2015



Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR limeanza jijini Dar es Salaam huku changamoto lukuki zikishuhudiwaikiwemo ukosefu wa mashine kwa baadhi ya vituo hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kujaza fomu peke yake bila kupigwa picha. Kwenye vituo mbalimbali ambapo zoezi hilo lilikuwa likifanyika kumekuwa na misururu mirefu ya watu na wengi wao wamelalamikia kitendo cha kuamka alfajiri ili kuwahi foleni lakini waandikishaji wakachelewa kuanza zoezi na hata zoezi lilipoanza wakashindwa kuandikisha kwa madai ya mashine kuwa mbovu.

Wakurugenzi wa manispaa ya Ilala na Kinondoni wamezungumzia malalamiko hayo ambapo mbali na kukiri kuwepo kwa mapungufu katika zoezi zima kwa upande wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilala mbali na changamoto zilizotokana na mashine amesema tatizo kubwa lililojitokeza ni wafanyabiashara kutaka kujiandikishia maeneo yao ya bishara wakati wanatakiwea kujiandikia wanakoishi huku akielezea hatua wanazochukuwa kukabiliana nazo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bw Musa Nati amesema tatizo lililojitokeza la mashine kutokufika kwa wakati kwenye baadhi ya vituo limetokana na uchache wa mashine ambapo walitarajia kupata mashine 1412 lakini wakapata 1312 kukawepo na upungufu wa mashine 100 na kwamba kuanzia sasa watu watakuwa wanapewa namba kulingana na idadi ya uandikishaji kwa siku.

Baada ya changamoto zilizojitokeza kwenye zoezi la uandikishaji mikoani,Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi aliwahakikishia wana Dar es Salaam kuwa mapungufu yaliyojitokeza awali mikoani hayawezi kujitokeza jijini hapa kwani mashine zote zitatumika kuandikisha.

0 comments: