Wednesday, July 22, 2015

Wednesday, July 22, 2015

MAMIA ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma leo walijitokeza kumuaga na kumzika Mbunge wa Viti Maalum Mkoani hapa Mariam Mfaki (69) aliyefariki jana hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma alipokuwa akipata matibabu ya maradhi ya saratani ya damu.
Hata hivyo ni mbunge mmoja tu alihudhuria msiba huo huku wabunge wengine wakiwa kwenye kampeni za kujinadi kuomba kuteuliwa na chama kuwa wagombea.
Mbunge aliyehudhuria msibani Felister Bura ambaye ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Dodoma.
Akitoa salamu Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema Marehemu Mfaki alikuwa ni kiongozi muwajibikaji ambaye alikuwa akishughulikia matatizo ya wananchi na kuyafikisha mahali panapohusika.
“Alikuwa ni mtu mwenye upendo wakati wote na alikuwa ni mtu mwenye kujituma, licha ya kuumwa alitaka kwenda bungeni, kuna wakati nilikwenda kumuona akaniambia nataka niwepo wakati Rais akilivunja bunge nikamwambia apumzike kwani ni mgonjwa” alisema
Alisema alikuwa akijali kila mtu na alikuwa tayari kupokea matatizo ya wengine.
“Alikuwa na moyo wa kujali kila mtu pia alikuwa ni mama aliyekuwa amekumbatia watoto wake kwa nguvu sana hata unapofika nyumbani kwake utakuta imejaa watoto wenye upendo mkubwa’ alisema
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Felister Bura alisema alimfahamu marehemu Mfaki mwaka 2003  akiwa mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) na alimhamasisha sana kuwa Mbunge.
“Alituhamasisha katika mikutano yake mpaka nikahamasika na mwaka 2005 nikagombea Ubunge wa viti maalum na nikashinda” alisema
Alisema alifanya naye kazi vizuri alikuwa mpenda watu na mlezi wa wabunge wa Dodoma.
 Katika salamu zake, mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa alisema kazi za marehemu Mfaki zitaendelea kuheshimika na kuenziwa.
Katibu wa UWT, Taifa Amina Makilagi alisema marehemu alikuwa akifanya kazi zake bila ubaguzi wa kabila dini au rangi.
“Wakati nikiingia UWT nilipokelewa na mama Mfaki ambaye alikuwa akituasa namna ya kuongoza ili kuwakwamua wanawake.
Akisoma historia ya marehemu, Mkurugenzi Msaidizi Huduma kwa Wabunge Suleiman Mvunye alisema  Mfaki alizaliwa Novemba 26, 1946 katika Kijiji cha Pahi Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma na alipata elimu yake Kondoa na shule ya wasichana ya kati Singida.
Alisema marehemu alifanya kazi Serikalini kuanzia mwaka 1965 akiwa Ofisa maendeleo Wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za mitaa, baadae akahamia vyama vya ushirika kuanzia mwaka 1968 hadi 1972.
Alisema mwaka 1973 hadi 1976 alifanya kazi kama katibu wa UWT Wilaya ya Kondoa, pia mwaka 1984 hadi 1998 alifanya kazi kama katibu tarafa na kuanzia mwaka 1997 hadi 2007 alikuwa mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma.
Alikuwa Mjumbe wa NEC kuanzia 1970 hadi 2001, kuanzia mwaka 2000 hadi 2015 alikuwa mbunge wa viti maalum mkoa wa Dodoma.
Marehemu ameacha mume watoto sita na wajukuu 10 alizikwa shambani kwake eneo la Miuji manispaa ya Dodoma.

0 comments: