Azam FC wametwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuifunga mabao 2-0 Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
Azam FC inakuwa timu ya kwanza ya Tanzania nje ya Simba na Yanga SC kutwaa taji hilo Azam FC imewahi kushiriki kwa mara ya tatu tu mashindano hayo baada ya kufika fainali na kufungwa na Yanga SC 2-0 Dar es Salaam mwaka 2012 na kutolewa kwa penalti 4-3 mjini Kigali, Rwanda baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90 katika Robo Fainali na El Merreikh ya Sudan walioibuka mabingwa mwaka jana .
Mabingwa hao wanaotoka Azam Complex, Chamazi, Temeke jijini Dar es Salaam wameshinda mechi zake zote kuanzia Kundi C bila kuruhusu nyavu zake kuguswa hata mara moja tofauti na walipokutana na Yanga SC kwenye robo fainali na wakashinda kwa penalti 5-3 baada ya timu hizo kutoka suluhu kwenye dakika 90.
Baada ya kupita hatua hiyo Azam iliilaza KCCA 1-0.
Mashabiki wa Gor Mahia wakiwa na simanzi baada ya kufungwa na Azam FC
Kwa ushindi huo, Azam imejinyakula kitita cha dola za Kimarekani 30,000 (Sh. Milioni 60), wakati Gor Mahia ambao ni washindi wa pili wataambulia dola za kimarekani 20,000 (Sh. Miliioni 40).
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Louis Hakizimana wa Rwanda aliyesaidiwa na Nagi Ahmed wa Sudan na Suleiman Bashir wa Somalia, hadi mapumziko tayari Azam FC walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.
Bao hilo lilipatikana dakika ya 16, mfungaji akiwa John Raphael Bocco ‘Adebayor’ baada ya kumalizia kwa kichwa krosi ya Kipre Herman Tchetche kutoka wingi ya kulia.
Azam walionekana kutawala mchezo kwa dakika 20 za mwanzo, lakini baada ya hapo kasi yao ikapunguzwa na uchezaji wa rafu wa Gor Mahia ambao hawakuchukuliwa hatua yoyote na refa Hakizimana.
Wachezaji wa Gor walikuwa wakiwapiga viwiko na mateke wachezaji wa Azam FC na kuanguka chini wakitokwa hadi damu, lakini hiyo haikumfanya refa Hakizimana japo kutoa kadi ya njano.
Medie Kagere alikaribia kuisawazishia Gor Mahia dakika ya 22 kama si umahiri wa beki kisiki wa Azam FC, Serge Wawa Pasacal.
Kipindi cha pili, Azam walianza na mabadiliko kwa kumtoa winga Farid Mussa Malik ambaye nafasi yake lichukuliwa na beki David Mwantika, mabadiliko ambayo inaonekana yalilenga kuimarisha ulinzi kwa timu na hivyo kupunguza kasi ya Gor Mahia ambao awali walijaribu kuutawala mchezo.
Dakika ya 64 Kipre Herman Tchetche akaifungia bao la pili kwa shuti la mpira wa adhabu lililompita kama mshale kipa wa Gor Mahia, Boniphace Olouch.
Faulo hiyo ilitokana na beki Harun Shakava kumuangusha beki wa Azam FC, Shomary Kapombe nje kidogo ya boksi.
Mchezo uliotangulia mchana wa leo, KCCA ya Uganda iliifunga 2-1 Khartoum N ya Sudan na kumaliza katika nafasi ya tatu.
Kikosi cha Azam FC kilichoanza leo kilikuwa hivi : Aishi Manula, Aggrey Morris, Morald Said, Pascal Wawa, Farid Mussa/Erasto Nyoni dk46, Shomari Kapombe, Jean Mugiraneza, Himid Mao, Ame Ali/Frank Domayo dk69, John Bocco na Kipre Tchetche/dk88.
Gor Mahia; Boniphace Olouch, Mussa Mohammed, Sibomana Abouba, Harun Shakava, Karim Nzigiyimana, Innocent Wafula/Enock Agwanda dk83, Khakid Aucho, Godfrey Walusimbi, Medie Kagere/George Odhiambo dk83, Michael Olunga na Erick Ochieng/Ali Abondo dk74.
Gor Mahia; Boniphace Olouch, Mussa Mohammed, Sibomana Abouba, Harun Shakava, Karim Nzigiyimana, Innocent Wafula/Enock Agwanda dk83, Khakid Aucho, Godfrey Walusimbi, Medie Kagere/George Odhiambo dk83, Michael Olunga na Erick Ochieng/Ali Abondo dk74.
0 comments:
Post a Comment