Wednesday, August 12, 2015

Wednesday, August 12, 2015

Baada ya kujiuzulu kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF nimerejea katika shughuli za utafiti. Tangu mwaka 2011 nilipokutana na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, nilimueleza nia yangu ya kufanya utafiti wa nini Tanzania inaweza kujifunza kutoka Rwanda.

Sikupata fursa ya kufanya utafiti huo. Baada ya kuamua kun’gatuka  uongozi wa siasa, nimepata fursa ya kuendelea na utafiti huo kwa lengo ya kutoa ushauri wa mambo ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka Rwanda bila kuathiri harakati za kujenga demokrasia na kuheshimu haki za binadamu.

Mtanzania yeyote anapofika Kigali kwa mara ya kwanza atastaajabu usafi wa mji na uzuri wa barabara. Hakuna takataka na huwezi kuona mifuko ya plastiki mitaani. Utengenezaji na uagizaji wa mifuko ya plastiki umepigwa marufuku. Hakuna maeneo yenye vibanda vya ovyo ovyo (slums). Mji una amani na utulivu. Unaweza kutembea usiku bila kuogopa kuporwa au kuvamiwa na vibaka. Kigali ni mji wenye amani lakini pia una askari wengi mitaani wenye nidhamu. Hata vijijini hakuna nyumba zilizoezekwa kwa nyasi.


Wananchi wa Rwanda chini ya uongozi wa Rais Paul Kagame wamefanikiwa kuibadilisha nchi iliyokumbwa na mauaji ya kimbari mwaka 1994, kuwa nchi yenye amani na utulivu.  Katika kipindi cha siku 100 kuanzia Aprili 7 1994, wananchi milioni moja waliuawa. Idadi ya watu nchini Rwanda mwaka 1994 ilikuwa milioni saba.

Pamoja na watu milioni moja kuuawa, milioni mbili walilazimika kuwa wakimbizi. Kulikuwa na watoto wengi yatima wasiokuwa na ndugu yeyote. Katika historia ya mauaji ya kimbari hakuna nchi iliyoshuhudia mauaji ya watu wengi kwa muda mfupi kama ilivyotokea Rwanda. Kurejesha amani na utulivu peke yake ni mafanikio makubwa.

Rwanda pia imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii. Kati ya mwaka 2000 na 2014, pato la taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 7.7 kila mwaka. Wanyarwanda milioni 1 wamefanikiwa kujinasua kutoka kwenye lindi la umaskini wa kutupwa. Katika kipindi hiki wastani wa pato la kila mwananchi limeongezeka karibu mara mbili licha ya kuwa na kasi ya juu ya ongezeko la idadi ya watu.

Hakuna nchi iliyofanikiwa kurudisha amani na kukuza uchumi kwa muda mfupi baada mauaji makubwa na kusambaratika kwa taifa kama ilivyofanya Rwanda. Mafanikio haya yalitegemea misaada ya fedha kutoka nchi wahisani. Serikali ya Rwanda iliweza kutumia misaada hiyo vizuri. Zaidi ya hapo imeweka mkakati wa kupunguza kutegemea misaada ya nje.

Mwaka 2000 bajeti ya Serikali ya Rwanda ilitegemea misaada kwa asilimia 48.3. Ilipofika mwaka 2013, kutegemea misaada ya nje katika bajeti ya serikali kumepungua na kufikia asilimia 30.2.

Rwanda imejitahidi  katika kupambana na ufisadi mkubwa na rushwa ndogondogo. Baadhi madereva wa malori kutoka Tanzania waliotoa rushwa kwa askari wa barabarani wamefikishwa mahakamani na kufungwa.

Taarifa ya Shirika la KimaTaifa (Transparency International) linalochunguza rushwa linaonyesha kuwa mwaka 2014, Rwanda ilipata alama 49 kati ya 100 na kuwa nchi ya 55 kati ya nchi 175 kwa kuwa na rushwa kidogo. Tanzania ilipata alama 31 kati ya 100 na kuwa nchi ya 119.

Rwanda ni nchi ndogo isiyokuwa na ufukwe wa bahari lakini imefanya marekebisho ya sera zake na hivi sasa ni nchi ya tatu kwa ushindani wa kiuchumi katika bara la Afrika baada ya Mauritius na Afrika ya Kusini. Tanzania ni ya 21. Katika nchi 144 zinazofanyiwa tathmini ya ushindani wa kiuchumi, Rwanda ni ya 62 na Tanzania ni ya 121.

Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu wepesi wa kufanya biashara ya mwaka 2014 inaonyesha Rwanda ni nchi ya 32 kati ya nchi 189 wakati Tanzania ni nchi ya 145. Mwaka 2005 Rwanda ilikuwa ya 158. Tovuti ya Rais Kagame inaonyesha kuwa inachukua saa sita kuanzisha na kusajili kampuni. Nchini Tanzania inachukua siku 26.

Wastani wa miaka ya kuishi umeongezeka kutoka miaka 51mwaka 2000 na kufikia miaka 65 mwaka 2012. Asilimia 73 ya Wanyarwanda wana bima ya afya. Watoto wote wanajiunga na shule za msingi na asilimia 72.7 wanamaliza shule za msingi.

Rwanda imefanikiwa  katika kuleta usawa wa jinsia. Asilimia 64 ya wabunge ni wanawake. Zaidi ya theluthi moja ya mawaziri ni wanawake.
Matumizi ya kompyuta na mtandao yanaanzia shule za msingi. Katika nchi yenye eneo la kilomita za mraba 24,670, imetandaza nyaya za mtandao wa intaneti kilomita 2229.

Rais Kagame ni msimamizi wa karibu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hasumbuliwi na itikadi anajali matokeo. Ana kumbukumbu ya mambo mengi yanayoendelea Rwanda. Kwa mfano anajua watu wazima wangapi wataotarajiwa kufundishwa kusoma na kuandika katika kila wilaya. Au ng’ombe wangapi watakaopandishwa na mbegu bora katika eneo lipi.

 Viongozi wa serikali wanaingia na kuweka saini mkataba unaoitwa ‘imihigo’ kwa Kinyarwanda unaoeleza majukumu watakayoyatekeleza. Mikataba hii pia inawekwa saini na Rais Kagame mwenyewe. Usipotekeleza mkataba wako unapoteza kazi yako. Dhana ya imihigo inatokana na utamaduni wa Rwanda wa mtu kutoa ahadi katika jamii anayoishi ya kutekeleza majukumu aliyopanga na asipofanya hivyo jamii inamdharau na anakosa heshima.

Mpango Mkakati wa Rwanda wa kujenga uwezo wa utekelezaji (Strategic Capacity Building Initiative) unalenga kujenga uwezo wa serikali kutekeleza vipaumbele vichache lakini muhimu katika kuchochea maendeleo. Sekta zinazopewa kipaumbele na mpango huu ni kilimo, nishati, madini na uwekezaji.

Mkakati huu unazingatia malengo ya mpango wa pili wa maendeleo wa Rwanda unaolenga kubadilisha mfumo wa uchumi wa Rwanda na kuongeza tija, kuongeza uzalishaji sekta ya kilimo na kuleta maendeleo vijijini, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha utawala bora na uwajibikaji.

Ni rahisi kuhitimisha kuwa maendeleo yaliyopatakana Rwanda ni matokeo ya kuwa na kiongozi mwenye dira na mamlaka ya kidikteta. Haiwezekani Rais kwenye nchi yenye mfumo wa demokrasia kuweza kupata mafanikio yaliyopatikana Rwanda. Kuwa na mipango inayoeleweka na kuisimamia kikamilifu hakuitaji kuwa na Rais dikteta. Kunahitaji rais mwadilifu na muwajibikaji. Mfumo imara wa demokrasia unahitaji uwajibikaji na uadilifu.

Ili tuwe na maendeleo yanayowaletea neema wananchi wote tunahitaji demokrasia ya kweli na siyo utawala wa kidikteta. Demokrasia ya kweli inawapa fursa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi ulio huru na wa haki.

Hata hivyo haitoshi kuwa na uchaguzi huru. Serikali iliyochaguliwa lazima iwajibike kwa wananchi. Asasi muhimu za serikali inayowajibika na utawala bora ni pamoja na Bunge lenye mamlaka ya kuisimamia na kuiwajibisha serikali, mahakama huru zinazotenda haki, tume huru ya uchaguzi, mkaguzi na mdhibiti wa mahesabu ya serikali, tume yenye uwezo wa kupambana na rushwa, utumishi serikalini wenye weledi, mfumo wa kodi na ukusanyaji mzuri wa mapato ya serikali na usimamizi mzuri wa matumizi ya serikali.

Bunge la Rwanda linaisimamia serikali, mbunge hawezi kuwa waziri
Tanzania ni tajiri wa mali ya asili kuzidi Rwanda. Tunaweza kukuza uchumi unaoongeza ajira na kuwaletea neema wananchi wote ikiwa tutakuwa na uongozi wenye dira na sera mwafaka na usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Rais tutakayemchagua Oktoba 25 2015 anaweza kujifunza kutoka kwa Rais Kagame kuhusu usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mapema baada ya kuchaguliwa anaweza kukutana na Rais Kagame akajifunza uzoefu wa Rwanda kuhusu umuhimu wa kuweka vipaumbele na usimamizi wa utekelezaji.

0 comments: