Manispaa
ya Kinondoni jijini Dar es salaam imethibitisha uwepo wa ugonjwa wa
kipindupindu ambapo hadi sasa wagonjwa watatu wameripotiwa kupoteza
maisha huku zaidi ya 34 wakiwa wamelazwa katika vituo vya Mwananyamala
na Mburahati jijini Dar es Salaam.
Wataalamu wa afya wanasema mazingira yanayozunguka
makazi ya kuishi ndiyo yanaweza kusababisha uwepo wa magonjwa ya
maambukizi kama kipindupindu huku ikisisitizwa, kula bila kunawa, kula
matunda hovyo, kutoka msalani bila kunawa,kunywa maji bila kuchemsha na
kugusana na mgonjwa wa kipindupindu ni kati ya sababu kuu zinazosambaza ugonjwa huu. Ikiwa ni siku moja tu baada ya kuripotiwa
kuingia kwa ugonjwa huu, mpangaji mmoja ambaye mwanae amepatwa na ugonjwa huo,
ametishiwa kufukuzwa anakoishi baada ya mwenye nyumba kuhofia huenda
familia yake ikakubwa na ugonjwa huo.
Jitihada mbalimbali zinachukuliwa kuwaokoa wagonjwa wa kipindupindu
katika hospitali za Mwananyamala na Mburahati na wauguzi wameendelea kuwasisitizia wananchi kuzidisha usafi hasa kipindi hiki cha mlipuko wa
ugonjwa huu wa kipindupindu.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt Azizi Msuya
amesema hadi sasa wamekwisha sambaza dawa katika kata zaidi ya 70
zinazozunguka kambi hizo ikiwa ni pamoja na kupulizia dawa za kuulia
vijidudu vya ugonjwa huo.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Mhandisi Mussa
Natty, amewatahadhalisha wakazi wa manispaa hiyo kuepukana na misongamano pamoja na kula chakula cha pamoja ili kuweza kuepuka uwezekano
wa kupata maambukizi ya ugonjwa huo.
Mpaka sasa zaidi ya wagonjwa 34 wamelazwa, mwananyamala ikiwa na wagonjwa 18 wakubwa wanne na watoto 14. Kituo cha
sinza kina wagonjwa 16 ambapo kati yao wanaume ni 13 wanawewake 3.
0 comments:
Post a Comment