Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) Bw. Edward Lowassa (pichani kulia), amewahimiza watanzania kutokubali kurubuniwa kuuza vitambulisho vyao kupigia vya kura, kwa kuwa hatua hiyo itaua mabadiliko chanya yanayokuja nchini.
Bw. Lowassa ameutoa wito huo mkoani Singida katika Majimbo ya Singida Magharibi, Singida Kaskazini, Iramba Mashariki na Iramba Magharibi, ambapo alipita kuomba kura na kuwanadi wagombea ubunge na madiwani katika majimbo hayo, huku akiwasisitiza wananchi kutokubali kurubuniwa kuuza vitambulisho vya kura kwa kuwa watauza utu wao.
Mh. Lowassa amewasisitiza wananchi kutambua kuwa mabadiliko ya kweli yataletwa na (UKAWA) kupitia sanduku la kura, na wao watahakikisha hakuna kura itakayoibiwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Mapema kabla ya Lowassa kupanda jukwaani,makada mbalimbali wa vyama vinavyounda (UKAWA), wamewahimiza wananchi kuwachagua wabunge na madiwani wanaounda umoja huo, kwani vyama hivyo vina lengo la kweli la kuleta mabadiliko nchini ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa upande wake mmoja wa wagombea ubunge kwa upande wa Singida Kaskazini Bw. David Djumbe amewaomba wananchi wampe kura ili aweze kutatua changamoto zilizopo katika jimbo hilo ambalo lilikuwa likiongozwa na waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu.
0 comments:
Post a Comment