Thursday, September 3, 2015

Thursday, September 03, 2015
Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi TACAIDS, imesema jumla ya watumishi 17,740 kutoka sekta ya umma wamejitokeza katika zoezi lililotekelezwa kati ya Septemba 2014 na Mei mwaka huu 2015, la upimaji wa afya zao kwa hiyari, lililozinduliwa rasmi mkoani Iringa na baadaye kutekelezwa katika mikoa kumi na miwili ya Tanzania Bara ikiwemo Iringa, Mbeya,Njombe na Pwani.

Mwenyekiti Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Fatma Mrisho,amebainisha hayo kabla ya zoezi la upimaji afya kwa wafanyakazi wa Tume hiyo jijini Dar es Salaam,ikiwa ni muendelezo wa zoezi hilo ambalo tayari limeshafanyika kwenye taasisi nane za serikali likilenga kupima jumla ya wafanyakazi 350,000 kutoka sekta ya umma na binafsi.

Dk Mrisho amesema, kati ya watumishi hao 17,740,wanaume walikuwa 10,149 sawa na asilimia 57 na wanawake 7,591 sawa na asilimia 43 ambapo waliogunduliwa kuwa na maambukizi ya  virusi vya ukimwi (VVU),walikuwa 752 sawa na asilimia nne,wanaume walikuwa 366 sawa na asilimia 49 na wanawake 386 sawa na asilimia 51.

Mwenyekiti huyo wa TACAIDS,amesema, takwimu hizo zinaonyesha mwitikio wa akina baba ni sawa na akina mama tofauti na miaka ya nyuma ambapo mwitikio mkubwa ulikuwa ni wa akina mama .

Wakati huo huo,Tume imesema  kwamba, maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa ujumla yamepungua ikilinganishwa na kufikia asilimia 5.1 kwa sasa.

0 comments: